Jenerali Qaani: Iran itawashangaza wengi katika medani ya vita
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema: Mrengo wa Haki utaendelea kuwa na uwezo na nguvu zaidi kila siku, na kwamba Iran itawashangaza wengi katika uwanja wa vita na utawala wa Kizayuni pamoja na Marekani.
Brigedia Jenerali Esmail Qaani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameandika katika ujumbe uliotumwa kwa makamanda, viongozi na wapiganaji wa mrengo wa muqawama kwamba: Hatua zenu za kujitolea, zenye ikhlasi, ujasiri na za dhati katika vita dhidi ya Marekani inayotenda jinai na utawala wa Kizayuni unaoua watoto wadogo zinasifiwa na kila mtu na kuibua furaha miongoni mwa waumini na wapigania uhuru kote ulimwenguni na wakati huo huo kuibua hasira, mshangao na hofu kubwa miongoni mwa maadui.
Amesisitiza kuwa: "Leo ni wazi kwa kila mtu kwamba, Mrengo wa Muqawama una uwezo wenye thamani kubwa sana ambao umeingia vitani dhidi ya Marekani mtenda-jinai na utawala wa Kizayuni unaoua watoto, kwa kujitegemea na kwa maamuzi na mipango yake ya busara kwa ajili ya kuitetea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mrengo huu kufikia sasa umetekeleza operesheni zenye mafanikio makubwa na utaendelea kuwashangaza wengi katika siku zijazo."