Askari wa Marekani watoweka wakati wa mazoezi ya kijeshi Morocco
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138148-askari_wa_marekani_watoweka_wakati_wa_mazoezi_ya_kijeshi_morocco
Askari wawili wa Jeshi la Marekani waliokuwa wakishiriki katika mazoezi ya kijeshi karibu na mji mmoja kusini-magharibi mwa Morocco wameripotiwa kutoweka, na hadi sasa hawajulikani waliko.
(last modified 2026-05-04T09:37:12+00:00 )
May 04, 2026 09:30 UTC
  • Askari wa Marekani watoweka wakati wa mazoezi ya kijeshi Morocco

Askari wawili wa Jeshi la Marekani waliokuwa wakishiriki katika mazoezi ya kijeshi karibu na mji mmoja kusini-magharibi mwa Morocco wameripotiwa kutoweka, na hadi sasa hawajulikani waliko.

Hayo ni kwa mujibu wa Kamandi ya Kijeshi ya Marekani barani Afrika (AFRICOM) na Jeshi la Morocco. AFRICOM ilieleza kuwa wanajeshi hao walionekana mara ya mwisho jioni ya Jumamosi karibu na eneo la mafunzo la Cap Draa, lililo karibu na Bahari ya Atlantiki, karibu na mji wa Tan-Tan—ukanda wenye miamba mikali na jangwa ambako sehemu ya mazoezi hayo hufanyika.

Imedaiwa kuwa wanajeshi hao hawakuwa katika mazoezi wakati walipopotea; “huenda walikuwa wanaogelea” katika eneo ambalo Mto Oued Draa unaingia Bahari ya Atlantiki, takribani kilomita 25 kaskazini mwa Tan-Tan.

Majina ya wanajeshi hao waliopotea hayajatangazwa hadi sasa.

Mazoezi hayo, yanayojulikana kama 'Simba wa Afrika', yalianzishwa mwaka 2004, na ni miongoni mwa mazoezi makubwa zaidi ya kijeshi yanayoongozwa na Marekani barani Afrika, ambayo Washington hudai kuwa yanalenga kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji na utayari wa vikosi shiriki pamoja na washirika wa NATO.

Mazoezi hayo mwaka huu yalianza Aprili 27 na yanaendelea hadi Mei 8 katika nchi nne: Morocco, Tunisia, Senegal na Ghana. Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii barani Afrika wamekosoa kufanyika kwa mazoezi hayo ya kijeshi barani Afrika wakati jeshi la Marekani linahusika na vita dhidi ya Iran, ambavyo vimesababisha matatizo makubwa ya kiuchumi barani Afrika.