Israel yafuta mpango wa kushambulia Beirut baada ya onyo kali la Iran
Utawala wa Israel umeachana na mpango wake wa kufanya mashambulizi makali ya ya kijeshi dhidi ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Haya yameelezwa siku ya Jumatatu na Rais wa Marekani, Donald Trump, kufuatia onyo kali kutoka kwa Iran kwamba haitavumilia wimbi jipya la uvamizi dhidi ya Beirut, hatua ambayo ingekiuka makubaliano ya kusitisha vita kati ya Iran na Marekani.
Kupitia ujumbe alioandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social siku ya Jumatatu, Trump alisema alikuwa na mazungumzo “yenye tija kubwa” na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye mapema siku hiyo alikuwa ameliagiza jeshi la utawala huo kufanya mashambulizi katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, hasa katika eneo la Dahiyeh ambalo ni ngome ya harakati ya Hizbullah.
Katika taarifa yake hiyo, Trump alisema: “Hakutakuwa na wanajeshi watakaoelekea Beirut, na wanajeshi wowote waliokuwa njiani wamesharudishwa nyuma.”
Mtawala huyo wa Marekani amedai pia kuwa amefanikiwa kupata makubaliano ya pembeni na harakati ya Hizbullah. Aliongeza kuwa: “Vilevile, kupitia wawakilishi wa ngazi za juu, nilifanya mazungumzo mazuri sana na Hizbullah, nao wamekubali kuwa mapigano yote yatasimama, kwamba Israel haitawashambulia, na wao hawataishambulia Israel.”
Matamshi hayo ya Trump yalikuja saa chache baada ya makamanda wa kijeshi wa Iran kutoa onyo kali kwa Israel na washirika wake, wakitangaza kwamba majeshi ya Iran yatajibu mapigo dhidi ya uvamizi wowote unaoendelea wa utawala huo huko Lebanon.
Makao Makuu ya Kijeshi ya Iran yaliwaonya walowezi wa Israel wanaoishi maeneo ya kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kujiandaa kuondoka, iwapo Israel itatekeleza vitisho vyake vya kushambulia maeneo ya kusini mwa Beirut kwa kisingizio cha kulenga maeneo ya Hizbullah.
Taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Iran ambayo ni maarufu kama Kamandi ya Khatam al-Anbiya, ilielezwa kuwa: “Kutokana na utawala huo kukiuka makubaliano ya kusitisha mapambano mara kwa mara, iwapo kitisho hiki kitatekelezwa, tunawaonya wakaazi wa maeneo ya kaskazini na vituo vya kijeshi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuondoka mara moja kama hawataki kupata madhara.”
Iran inasisitiza kuwa makubaliano ya kusitisha vita na Marekani, yaliyofikiwa kwa upatanishi wa Pakistan mnamo tarehe 8 Aprili, yanajumuisha kusitishwa kwa uadui katika pande zote, ikiwemo Lebanon.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alisisitiza tena siku ya Jumatatu kuwa makubaliano hayo yanahusisha “pande zote, ikiwemo Lebanon,” akionya kuwa ukiukaji wowote upande mmoja utachukuliwa kama ukiukaji wa makubaliano mapana ya kusitisha mapambano.