Iran yapinga 'matakwa ya kupita kiasi' katika mazungumzo au kusitisha mapigano
-
Mohsen Rezaei
Mshauri wa Masuala ya Kijeshi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei amesema kuwa Tehran haitairuhusu Marekani kuwasilisha matakwa ya kupita kiasi, iwe ni katika mazungumzo au wakati wa mchakato wa kusitisha mapigano.
Mohsen Rezaei ameonya kuwa kitendo chochote cha uchokozi kitakabiliwa na mashambulizi mtawalia ya makombora na ndege zisizo na rubani. Rezaei ameeleza haya katika ujumbe aliotuma katika akaunti yake ya X.
"Si katika mazungumzo au katika mchakato wa kusitisha mapigano, hatutairuhusu Marekani kuwasilisha matakwa ya kupita kiasi," ameandika Rezaei.
Ameongeza kuwa: Ufyatuaji risasi au uchokozi wowote utajibiwa kwa kuvurumisha makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya adui. Historia haitarudi nyuma, na mchokozi ataadhibiwa bila kuchelewa.
Jumanne wiki hii Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitangaza kuwa limeshambulia kwa makombora na droni makao makuu ya Kikosi cha Tano cha Jeshi la Wanamaji la Marekani nchini Bahrain na kambi ya Jeshi la Anga la Marekani nchini Kuwait na maeneo mengine ya kijeshi ya nchi hiyo katika Ghuba ya Uajemi.
IRGC ilifanya mashambulizi hayo kulipiza kisasi mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya meli ya Iran katika Ghuba ya Oman na kwa hujuma ya Washington dhidi ya mnara wa mawasiliano kusini mwa kisiwa cha Qeshm nchini Iran.
Mashambulizi haya ni ya tatu kuwafanywa na Iran dhidi ya kambi za Marekani nchini Kuwait katika muda wa wiki moja.