Iran yaonyesha mabaki ya ndege za kivita za Marekani na Israel ilizozitungua +Video
Iran imeonyesha sehemu za vifaa vilivyopatikana kutoka ndege za kivita zisizo na rubani (droni) za Marekani na Israel, pamoja na ndege ya kivita ya F-15 ambazo zilitunguliwa kwa mifumo ya ulinzi ya Iran wakati wa vita. Mifumo ya ulinzi iliyotumika kutungua ndege hizo za adui imeundwa hapa nchini.
Afisa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameonekana akitoa ufafanuzi kuhusu zana hizo za adui katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB), yaliyorekodiwa katika moja ya kambi za chini ya ardhi za IRGC na kurushwa hewani Ijumaa
Sehemu kubwa za droni kadhaa za Marekani na Israel, zikiwemo MQ-9 Reaper, Hermes 900 na Hermes 450, pamoja na vifaa vya kiufundi kutoka MQ-9 na ndege ya kivita ya Marekani aina ya F-15, zilionyeshwa katika ripoti hiyo.
Afisa huyo mwandamizi wa Kikosi cha Anga cha IRGC pia amesema uzalishaji na uwasilishaji wa mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran umeendelea bila kukatizwa baada ya vita vya siku 40 vya uchokozi wa Marekani na Israel.
Ameongeza kuwa: “Kutokana na hatua zilizochukuliwa kabla ya vita, zaidi ya asilimia 85 ya miundombinu ya uzalishaji wa mifumo ya ulinzi wa anga inayotengenezwa na Shirika la Jihadi ya Kujitosheleza la Kikosi cha Anga cha IRGC ilihifadhiwa.”
Akiashiria ndege ya kivita ya Marekani aina ya F-15, ambayo ilipigwa kwa kombora la Iran tarehe 3 Aprili wakati wa operesheni iliyotekelezwa na vikosi vya ulinzi wa anga vya Kikosi cha Anga cha IRGC, amesema: “Ndiyo, ndege hii ya kivita ilipigwa kwa mfumo mpya wa ulinzi wa anga na kombora jipya, kwa kutumia mbinu ya Kiirani kikamilifu.
Nukta nyingine muhimu ni kuwa droni zilizotunguliwa zilikuwa na mfumo wa mawasiliano ya interneti wa Starlink kwa ajili ya kuwasiliana na majasusi wa Marekani na Israel waliokuwa wakitumia mifumo kama hiyo ndani ya Iran.
Vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vilianza tarehe 28 Februari. Katika kujibu, Vikosi vya Ulinzi vya Iran vililenga shabaha maeneo muhimu ya kimkakati ya Marekani na Israel katika maeneo mbalimbali ya kanda, na kuweka vikwazo kwa usafiri wa kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Baada ya siku arobaini, tarehe 8 Aprili, maadui walilazimika kukubali usitishaji kufuatia msimamo imara wa Iran na operesheni zake za kulipiza kisasi zilizofanikiwa.
Tarehe 17 Juni, Iran na Marekani zilitia saini Hati ya Maelewano (MoU) iliyosimamiwa na Pakistan, kwa lengo la kusitisha uhasama wote na kuandaa mazingira ya mazungumzo zaidi.
Hata hivyo, Washington imekiuka vipengele vyote vya maelewano hayo, hali iliyosababisha Iran kutoa jibu thabiti.