Oct 18, 2016 03:09 UTC
  • Uzalishaji mafuta nchini Iran warejea katika kiwango cha kabla ya vikwazo

Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, baada ya kuanza utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 ambayo ni maarufu kwa jina la makubaliano ya JCPOA, uzalishaji wa mafuta wa Iran umekaribia kiwango cha kabla ya vikwazo, yaani mapipa milioni nne na laki mbili kwa siku.

Bijan Namdar Zangeneh, Waziri wa Mafuta wa Iran amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akisema mbele ya waandishi wa habari hapa mjini Tehran kuwa, kiwango cha uzalishaji mafuta ya Iran ni karibu mapipa milioni nne kwa siku hivi sasa, na hii ina maana ya kukaribia mno kiwango cha uzalishaji wa mafuta ya Iran kabla ya kuwekewa vikwazo vya kidhulma na madola ya Magharibi kwa sababu ya miradi yake ya amani ya nyuklia.

Waziri wa Mafuta wa Iran ameongeza kuwa, sasa hivi hakuna tena vizuzi vya kibenki kwa ajili ya mikataba mipya na kwamba juhudi za wizara yake hivi sasa zimeelekezwa kwenye kuondoa vizuizi vyovyote vinavyoweza kutokea katika siku za usoni.

Sekta ya mafuta nchini Iran

 

Mapema mwezi huu wa Oktoba, Mfuko wa Fedha Duniani IMF ulisema kwamba, uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unakuwa kwa kasi kubwa kufuatia kutekelezwa makubaliano ya nyuklia yanayofahamika kama Mpango Kamili ya Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Ripoti ya IMF iliyotolewa siku ya Jumatatu ya tarehe 3 mwezi huu wa Oktoba ilisema kuwa, katika kipindi cha miezi sita ya kwanza kuondolewa vikwazo, uchumi wa Iran umekuwa kwa kiwango kikubwa na cha kuridhisha. Kadhalika ripoti hiyo ya Mfuko wa Fedha Duniani ilisema kuwa, hatua ya Iran ya kuongeza kiwango cha uzalishaji na uuzaji wa mafuta nje ya nchi imesaidia kudhibiti kuporomoka bei ya mafuta duniani.

Tags