Iran: Wananchi wamevunja njama zote za maadui
Waziri wa Usalama wa Taifa wa Iran amesema kuwa, kushiriki vilivyo wananchi katika nyuga tofauti kumefanikiwa kuvunja njama zote za maadui.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Sayyid Mahmoud Alavi akisema hayo jana (Jumamosi) katika kongamano la taifa la masuala ya usalama na wananchi hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, kitengo cha habari cha Wizara ya Usalama wa Taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kiungo muhimu mno baina ya wananchi na wizara hiyo.
Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kutoa pigo kubwa kwa adui kupitia kitengo cha habari cha wizara hiyo ya usalama wa taifa.
Alavi amebainisha pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo wa wananchi wenye uungaji mkono kamiili wa wananchi katika nukta zake zote. Amesisitiza kuwa, kama tunaona leo hii kwamba madola ya kibeberu hayathubutu kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tujue kuwa hayo ni matunda ya kushiriki vilivyo wananchi wa Iran katika nyuga zote zinazohusiana na nchi yao.
Ikumbukwe kuwa, mwezi Julai mwaka huu, Sayyid Mahmoud Alavi aliwaambia wandishi habari hapa mjini Tehran kwamba mwishoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhani wizara yake iliwatia nguvuni wanachama watano hadi sita wa makundi ya kigaidi waliokuwa na nia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi humu nchini. Alisema, magaidi hao walipanga kufanya mashambulizi ya kigaidi katika usiku wa Lailatul Qadr na katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika miji mbalimbali ya Iran, lakini wizara yake ilisambaratisha njama hizo.