Udharura wa kutoa jibu waungaji mkono wa magaidi wanaotumia silaha za kemikali
Mwakilishi wa Iran katika Shirika Linalopiga Marufuku Silaha za Kemikali (OPCW) ameeleza kuwa nchi zinazoyaunga mkono makundi ya kigaidi yanayotumia silaha za kemikali zinapasa kutoa jibu kuhusu suala hilo.
Kongamano la 21 la Nchi Wanachama wa Mapatano ya Silaha za Kemikali limeanza mkutano wake huko The Hague Uholanzi kwa kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Linalopiga Marufuku Silaha za Kemikali, wawakilishi wa ngazi ya juu wa nchi wanachama na taasisi zisizo za kiserikali. Akizungumza katika kongamano hilo jana huko The Hague Uholanzi, Alireza Jahangiri Mwakilishi wa Iran katika shirika la OPCW amekosoa ripoti zilizowasilishwa kuhusiana na utumiaji wa silaha za kemikali unaofanywa na makundi ya kigaidi huko Iraq na Syria yakiwemo makundi ya Daesh na Jabhatul Nusra.
Jahangiri amebainisha kuwa, nchi zinazoyaunga mkono makundi ya kigaidi ambazo zinafanikisha upatikanaji wa silaha za kemikali kwa ajili ya kutumiwa na makundi hayo dhidi ya raia wasio na hatia zinapasa kutoa majibu kuhusu hatua zao hizo. Mwakilishi wa Iran katika Shirika Linalopiga Marufuku Silaha za Kemikali (OPCW) pia ameashiria kuwepo vilema na majeruhi wa silaha za kemikali nchini Iran wapatao laki moja na kuongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitoa umuhimu maalumu kwa Mapatano ya Silaha za Kemikali na kutaka kutekelezwa kikamilifu vipengee vya mapatano hayo.