Jahangiri: Marekani imekiuka muafaka wa kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20758-jahangiri_marekani_imekiuka_muafaka_wa_kimataifa
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali hatua ya Baraza la Seneti la Marekani ya kupitisha muswada wa kurefusha kwa muda wa miaka 10 mingine Sheria ya Vikwazo Dhidi ya Iran (ISA) na kusema kuwa, kitendo hicho mbali na kuonyesha kuwa Washington haina muamana, pia ni ukiukaji wa makubaliano ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2016 00:26 UTC
  • Jahangiri: Marekani imekiuka muafaka wa kimataifa

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali hatua ya Baraza la Seneti la Marekani ya kupitisha muswada wa kurefusha kwa muda wa miaka 10 mingine Sheria ya Vikwazo Dhidi ya Iran (ISA) na kusema kuwa, kitendo hicho mbali na kuonyesha kuwa Washington haina muamana, pia ni ukiukaji wa makubaliano ya kimataifa.

Es'haq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran aliyasema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, hatua hiyo ni dhihirisho kuwa Marekani katu haiheshimu mikataba na makubaliano  ya kimataifa kwa msingi wa  wajibu wake wa kimataifa.

Amesema makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama JCPOA, ni matundo ya mazungumzo ya kina na ya muda mrefu kati ya Iran na nchi za kundi 5+1 kwa baraka kamili ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; na hivyo kuyavunja, sio tu ni kuihujumu Iran moja kwa moja, bali ni kukanyaga muafaka wa kimataifa.

Muswada huo unasubiri saini ya Rais wa Marekani anayeondoka madarakani Barack Obama. Ofisa mmoja mwandamizi katika Ikulu ya Marekani (White House) amesema Obama anatazamiwa kusaini muswada huo na kuwa sheria katika kipindi cha siku 10 zijazo.

 

Kongresi ya Marekani

Hii ni katika hali ambayo, Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran, imeanza kujadili hoja ya dharura  kwa lengo la kuitaka serikali ya Tehran ianzishe tena shughuli zote za nyuklia kwa malengo ya amani kama ilivyokuwa kabla ya mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezajiwa JCPOA baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.

Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilitia saini mapatano ya nyuklia ya JCPOA  Julai mwaka jana na kuanza kuyatekeleza Januari mwaka huu.