Zarif: Kipindi cha ubeberu wa Marekani Mashariki ya Kati kimepita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20833-zarif_kipindi_cha_ubeberu_wa_marekani_mashariki_ya_kati_kimepita
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, zama za ubeberu wa nchi za Magharibi hususan Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, zimepita na kuyoyoma.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 06, 2016 03:45 UTC
  • Zarif: Kipindi cha ubeberu wa Marekani Mashariki ya Kati kimepita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, zama za ubeberu wa nchi za Magharibi hususan Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, zimepita na kuyoyoma.

Dakta Muhammad Javad Zarif ambaye alikuwa akihutubia wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Peking nchini China amesema kuwa, baada ya kusambaratika Urusi ya zamani kulijitokeza taswira isiyo sahihi katika nchi za Magharibi kwamba huo ulikuwa ushindi kwa Wamagharibi na kwa mujibu wa taswira hiyo potofu Marekani ilifanya jitihada za kujitangaza kama dola kubwa pekee duniani. 

Zarif ameongeza kuwa, kwa kutumia taswira hiyo Marekani ilizishambulia na kuzivamia nchi kama Afghanistan na Iraq ili kuimarisha zaidi fikra ya dola kubwa pekee, lakini ukweli ni kuwa, zama za ubeberu unaotokana na tasiwi na fikra hiyo potofu zimepita na kuyoyoma.

Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, walimwengu wanakabiliana na changamoto nyingi kuanzia changamoto za mazingira, misimamo mikali, ugaidi na kadhalika na kwamba China kama kiungo muhimu, ina nafasi na mchango mkubwa katika kipindi cha sasa.

Dakta Zarif amesema, sababu kuu ya kujitokeza mitazamo mikali na ugaidi duniani ni hisi za chuki na kukosa matumaini vinavyosababishwa na mavamizi wa kigeni. Amesisitiza kuwa, ratiba za kiutamaduni na vyuo vikuu vinaweza kuwa njia bora ya kukabiliana na misimamo mikali na kwamba njia za kijeshi si utatuzi wa changamoto hiyo.