Larijani: Wafuasi wa dini zote wanatendewa haki nchini Iran
-
Dk Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, Katiba ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran imefanya uadilifu kwa kuwatendea haki wafuasi wa dini mbalimbali humu nchini.
Ali Larijani amesema hayo leo Jumatano wakati alipoonana na Wabunge Wakristo, Maashuri na Waarmenia wa Iran kwa mnasaba wa mwaka mpya wa 2017 na huku akiashiria namna watu wa dini zote wanavyoishi kwa usalama na amani nchini Iran amesisitiza kuwa: Wafuasi wa dini na madhehebu yote wanaangaliwa kwa jicho sawa na Katiba ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Vile vile amesema, Masih Issa AS na Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu ni wajumbe wa amani na utulivu na jukumu lao kuu ni kusimamisha uadilufu na kuenea mapenzi na maisha ya ufanisi baina ya watu kwa miongozo yao mitukufu.
Wabunge mbalimbali wa Wakristo wa Kiashuri, Kiarmenia Kaskazini na Wakristo wa Kiarmenia wa jimbo la kusini, wamesisitizia udharura wa kulindwa umoja na mshikamano katika jamii na matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iran kwenye kipindi nyeti kilichopo hivi sasa kwenye eneo hili.