Iran yaitahadharisha Marekani kuhusu makombora
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i24517-iran_yaitahadharisha_marekani_kuhusu_makombora
Waziri wa Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya Marekani kuhusu kubadilisha kadhia ya makombora halali ya Iran kuwa mchezo wa kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 31, 2017 10:00 UTC
  • Iran yaitahadharisha Marekani kuhusu makombora

Waziri wa Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya Marekani kuhusu kubadilisha kadhia ya makombora halali ya Iran kuwa mchezo wa kisiasa.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo mjini Tehran akizungumza na waandishi habari akiwa ameandamana na Jean-Marc Ayrault Waziri wa Mambo ya Nje ya Ufaransa. Zarif amesisitiza kuhusu uhalali wa mpango wa kujihami na makombora wa Iran na kusema: "Kama ambavyo pande zote katika mapatano ya nyuklia ya Iran (JCPOA) zilivyotangaza, kadhia ya makombora ya Iran haipo katika mapatano hayo ya nyuklia."

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amefafanua kuwa: "Katika azimio 2231 la Baraza la Usalama kuna ibara inayohusu maudhui ya makombora ya balisiki na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza msimamo wake wazi wakati wa kupitishwa azimio hilo."

Zarif amesema azimio hilo liliashiria kadhia ya makombora ya balisitiki ambayo yana uwezo wa kubeba silaha za nyuklia katika hali ambayo Iran imetangaza kuwa makombora yake hayana uwezo wa kusheheni silaha za nyuklia.

Jean-Marc Ayrault Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa (kushoto) na mwenzake wa Iran Mohammad Javad Zarif, Tehran, 31,01,2017

Aidha amesisitiza kuwa, katika suala la zana zake za kujihami, Iran haitafanya mazungmzo na nchi wala mtu yeyote. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya madola yaliyotia saini mapatano ya nyuklia ya JCPOA, hasa Marekani, yanakiuka mapatano hayo.

Wakati huo huo, Russia imesema hatua ya Iran ya kufanyia majaribio makombora yake ya balistiki haikiuki azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hii ni katika hali ambayo baraza hilo, kufuatia ombi la Marekani na utawala wa Kizayuni, limeitisha kikao cha dharura kujadili majaribio ya makombora ya Iran.