Larijani: Umoja wa kitaifa, suluhu ya migogoro ya Syria, Yemen
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema njia pekee ya kuipatia ufumbuzi migogoro inayoendelea kushuhudiwa katika nchi za Syria na Yemen ni mshikamano na umoja wa kitaifa.
Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran aliyasema hayo jana Jumamosi hapa mjin Tehran, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Sweden Kjell Stefan Löfven aliyeko safarini hapa nchini na kuongeza kuwa, uingiliaji wa kijeshi hauwezi kusuluhisha migogoro katika nchi hizo za Kiarabu.
Larijani amefafanua kuwa, suala la kubuniwa serikali za muungano wa kitaifa katika nchi hizo limekuwa likipuuzwa kwa muda mrefu na yumkini ndio dawa mjarabu ya migogoro katika nchi hizo za eneo hili la Mashariki ya Kati.
Spika wa Bunge la Iran amebainisha kuwa, moja ya matatizo ya baadhi ya nchi za eneo ni kuhujumu demokrasia na uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi nyingine mbali na kusahau jukumu lao la kuhakikisha kuwa amani, usalama na uthabiti unashuhudia katika kanda hii.
Ali Larijani ameongeza kuwa, ukosefu wa usalama unaoshuhudiwa katika eneo hili umesababishwa na uingiliaji wa kijeshi na kwamba iwapo madola ajinabi yangekuwa na irada thabiti ya kumaliza migogoro katika nchi za Syria na Yemen, yangetoa kipaumbele kwa suluhisho la kisiasa.