Zarif: Iran ni mshirika wa uhakika wa kibiashara kwa ajili ya Ulaya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran ni mshirika wa uhakika wa kibiashara kwa ajili ya Ulaya.
Dakta Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu diplomasia ya uchumi na miradi mikuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja mbalimbali, katika mezaduara ya majadiliano ya kiuchumi iliyofanyika mjini Munich, Ujerumani na kuhudhuriwa na wakuu wa jumuiya na mashirika makubwa ya Ujerumani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa Ulaya haijawahi kupata hasara kwa kushirikiana kiuchumi na kibiashara na Iran; na hata katika kipindi cha vikwazo pia Iran ilitekeleza ahadi zake zote ilizotoa kwa mashirika ya binafsi na ya serikali ya nchi za Ulaya, na kimsingi imekuwa na itaendelea kuwa mshirika wa uhakika na wa kuaminika wa kibiashara wa Ulaya kwa jumla na hasa hasa kwa Ujerumani.
Katika mezaduara hiyo, Ali Majedi, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Ujerumani alitangaza kuwa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Iran na Ujerumani unaweza kuongezwa zaidi hadi kufikia kiwango cha yuro bilioni sita, ambacho kwa uchache ni mara mbili zaidi ya kiwango cha sasa.../