Netanyahu aeleza wasiwasi wake kuhusu uwezo na nguvu ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28104-netanyahu_aeleza_wasiwasi_wake_kuhusu_uwezo_na_nguvu_ya_iran
Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo tishio kubwa zaidi kwa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 22, 2017 03:26 UTC
  • Netanyahu aeleza wasiwasi wake kuhusu uwezo na nguvu ya Iran

Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo tishio kubwa zaidi kwa Israel.

Benjamin Netanyahu ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis yaliyofanyika mjini Tel Aviv. Netanyahu amekariri madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran na kusema kuwa, Marekani na Israel zinakabiliwa na vitisho vya pamoja vinavyoongozwa na Iran na kwamba kuna ulazima wa hatari hiyo kuondolewa. Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel pia amesifu misimamo iliyo dhidi ya Iran ya serikali ya Marekani.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema Israel ni miongoni mwa washirika na marafiki wa siku nyingi za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, Washington inawajibika kulinda usalama wa Israel.

Netanyahu akitembelea majeruhi wa Daesh katika hospitali za Israel

Wakati huo huo Waziri wa Vita wa Israel, Avigdor Lieberman amekariri tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran katika mazungumzo yake ya mwenzake wa Marekani na kudai kuwa, Iran ndio muungaji mkono mkubwa zaidi wa ugaidi. Lieberman ametoa wito wa kuzidishwa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Madai hayo ya viongozi wa Israel dhidi ya Iran yametolewa wakati utawala huo wa Kizayuni daima umekuwa ukitangaza kuwa hautaacha kufanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kuyaunga mkono na kuyasaidia magenge ya kigaidi nchini Syria. Hivi karibuni pia mkuu wa shirika la ujasusi la Israel, MOSSAD, alikiri tena kwamba utawala huo unawapatia matibabu wapiganaji wa kundi la kigaidi la al Nusra katika hospitali za Israel.