Zarif: Ramadhani ni fursa kwa Waislamu kuimarisha umoja wao
(last modified Sun, 28 May 2017 13:56:37 GMT )
May 28, 2017 13:56 UTC
  • Zarif: Ramadhani ni fursa kwa Waislamu kuimarisha umoja wao

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja mwezi mtukufu wa Ramadhani kama fursa ya kipekee inayoweza kutumiwa na Waislamu kote duniani kwa ajili ya kuimarisha umoja na mshikamano wao.

Katika ujumbe wake wa Ramadhani uliotolewa leo Jumapili, Mohammad Javad Zarif amewataka Waislamu kutumia Ramadhani ya mwaka huu kujikumbusha kuhusiana na yale yanayowaleta pamoja kama Umma mmoja, chini ya Muumbaji Mmoja.

Dakta Zarif amewakumbusha Waislamu kuwa, historia ya ujio wa Uislamu ni funzo lenye mazingatio kuhusu nguvu ya umoja pasina kujali tofauti za kimadhehebu na kimitazamo.

Waumini wa Kiislamu wakitekeleza ibada ya Swala nchini India

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, Ramadhani ni mwezi maalumu kwa Waislamu kote duniani, ambapo wanaadhimisha na kutafakari kuhusu kuteremshwa Kitabu Kitukufu cha Qurani, kutoka mbinuni.

Ameongeza kuwa, katika hali ambayo ulimwengu wa Kiislamu umepasuka na kukabiliwa na tofauti zinazotokana na migogoro ya ndani na nje, viongozi wa Umma wana wajibu wa kuungana na kusisitizia umuhimu wa kutatuliwa hitilafu zilizopo kwa njia ya mazungumzo na sio vita na uhasama.