Zarif: Matamshi ya Trump kuhusu mashambulio ya kigaidi ya Tehran yanaudhi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30206-zarif_matamshi_ya_trump_kuhusu_mashambulio_ya_kigaidi_ya_tehran_yanaudhi
Dk. Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, matamshi ya rais wa Marekani, Donald Trump kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi ya mjini Tehran ni kejeli kwa wahanga wa mashambulizi hayo na yanaudhi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 08, 2017 11:05 UTC
  • Zarif: Matamshi ya Trump kuhusu mashambulio ya kigaidi ya Tehran yanaudhi

Dk. Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, matamshi ya rais wa Marekani, Donald Trump kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi ya mjini Tehran ni kejeli kwa wahanga wa mashambulizi hayo na yanaudhi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hayo leo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Tweeter ambapo ameandika: Tamko la (Ikulu ya Marekani) White House na vikwazo vya Baraza la Sanate la nchi hiyo katika wakati huu ambapo Iran inakabiliana na magaidi wanaoungwa mkono na vibaraka wa Marekani yanachukiza mno na kutia hasira na kwamba wananchi wa Iran hawawezi kukubaliana na madai ya nchi hiyo kuwa eti haina uadui wa wananchi wa taifa hili.

 

Kwa mara nyingine, Donald Trump ameituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na kusema kwa kejeli kwamba, eti nchi inayounga mkono ugaidi imekuwa muhanga wa shari yake mwenyewe. Jana Jumatano tarehe 8 Juni 2017, mji wa Tehran ulishuhudia mashambulizi mawili ya kigaidi katika Haram ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) na jengo la kiidara la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).

Hata hivyo askari wa kulinda usalama wa Iran waliwaangamiza haraka magaidi wote bila ya kuathiri harakati nyingine muhimu za maeneo hayo. Kwa mfano kikao cha wazi cha Bunge la Iran kiliendelea kama kawaida, bila ya kusita hata dakika moja. Raia 13 wa Iran wameuawa shahidi kwenye matukio hayo na wengine 43 wamejeruhiwa.

Rais wa Marekani, Donald Trump

 

Mapema leo asubuhi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika katika ukurasa wake wa Tweeter kuwa, watawala madikteta wanachukia kabisa demokrasia. Mamluki wao wamevamia kitovu cha demokrasia (yaani bunge la Iran) eneo ambalo linawachukiza sana madikteta hao.

Tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran hadi hivi sasa Marekani haijawahi hata mara moja kuficha uadui wake kwa taifa hili la Kiislamu.