Larijani: Hatua zote za Saudia ni kwa maslahi na manufaa ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30718-larijani_hatua_zote_za_saudia_ni_kwa_maslahi_na_manufaa_ya_israel
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameukosoa vikali utawala wa Aal-Saud kwa kushirikiana kufa kupona na utawala wa Kizayuni wa Israel na kubainisha kuwa, hatua zote za Riyadh katika eneo hili ni kwa maslahi na manufaa ya Tel Aviv.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 20, 2017 07:55 UTC
  • Larijani: Hatua zote za Saudia ni kwa maslahi na manufaa ya Israel

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameukosoa vikali utawala wa Aal-Saud kwa kushirikiana kufa kupona na utawala wa Kizayuni wa Israel na kubainisha kuwa, hatua zote za Riyadh katika eneo hili ni kwa maslahi na manufaa ya Tel Aviv.

Ali Larijani aliyasema hayo jana Jumatatu hapa mjini Tehran katika mkutano na mabalozi wa nchi za Kiislamu na kufafanua kuwa, kitendo cha Saudia kushirikiana na Israel kina taathira hasi na maafa kwa mataifa ya Kiislamu.

Larijani amesema: "Tumejitahidi kadri ya uwezo wetu kuwafanya watawala wa Aal-Saud waelewe kuwa, hatua zao za kuukingia kifua utawala haramu wa Israel haitakua na tija nyingine ghairi kuleta maafa kwa Umma wa Kiislamu; lakini jitihada zetu zimekuwa zikianguka kwenye sikio la kufa."

Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa, sera za Saudia katika masuala ya kieneo ni za kiuhasama na ndiposa Riyadh inashadidisha hujuma zake dhidi ya Yemen, kuzusha taharuki nchini Bahrain na sasa inaeleekeza mshale wake dhidi ya Qatar.

Spika wa Bunge la Iran, Ali Larijani

Amesema Saudi Arabia kwa upande mmoja inadai kuwa inapambana na ugaidi na kwa upande mwingine inayaunga mkono magenge ya kigaidi kama vile al-Nusra.

Dakta Larijani amezitahadharisha baadhi ya nchi za Kiislamu zinazoutegemea utawala wa Kizayuni wa Israel akisisitiza kuwa, hatua yao hiyo itakuwa na maafa makubwa kwa Umma wa Kiislamu ambao unafaa kuipa uzito na umuhimu kadhia ya Palestina.