Larijani: Wamarekani wanataka kuwafuta wapinzani wao kwa bwabwaja
Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa, Wamarekani wanatumia bwabwaja kama njia ya kutaka kuwafuta wapinzani wao.
Dakta Ali Larijani ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana katika siku ya mwisho ya safari yake nchini Korea Kusini amesema kuwa, vitisho vya Marekani vya kuiwekea Iran vikwazo zaidi ni maneno na bwabwaja zinazokaririwa na kuongeza kuwa: Tatizo ni kwamba maafisa wa Marekani wamejivika joho la wafanyabiashara.
Spika wa Bunge la Iran ameashiria pia hatua ya Marekani ya kukiuka makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 na kusema: Makubaliano hayo ni ya kimataifa ambayo yamepasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba kukiuka makubaliano hayo hakutakuwa na maslahi kwa Marekani. Amesisitiza kuwa kipindi cha nchi mmoja kutaka kuzitwisha nchi nyingine matakwa na misimamo yake kimepita, na kwamba nchi zote zinataka kuwa huru na kujitawala.
Vilevile ameilaumu Saudi Arabia kwa kuendelea kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kusema: Kundi la kigaidi la Daesh lina silaha zenye thamani ya dola bilioni 30 na inajulikana silaha hizo zimepatikana kutoka wapi.
Spika wa Bunge la Iran amesema wakati nchi hizo zikiyasaidia makundi ya kigaidi kama Daesh, Tehran iliharakia kuzisaidia serikali za Iraq na Syria kupambana na magaidi hao.