Spika wa Bunge Iran: Jumuiya za kimataifa zikabiliane na uhalifu wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i32218-spika_wa_bunge_iran_jumuiya_za_kimataifa_zikabiliane_na_uhalifu_wa_israel
Spika wa Bunge la Iran amelaani ukatili unaoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya raia wa Palestina katika mji mtakatifu wa Quds na Msikiti wa al Aqsa na ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kukabiliana ipasavyo na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Israel.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Jul 25, 2017 02:28 UTC
  • Spika wa Bunge Iran: Jumuiya za kimataifa zikabiliane na uhalifu wa Israel

Spika wa Bunge la Iran amelaani ukatili unaoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya raia wa Palestina katika mji mtakatifu wa Quds na Msikiti wa al Aqsa na ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kukabiliana ipasavyo na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Israel.

Dakta Ali Larijani amesema kuwa, kughusubiwa ardhi ya Palestina na Quds tukufu ni maumivu makubwa ya Umma mzima wa Kiislamu na kuongeza kuwa, Umma wa Waislamu unafuatilia kwa hisia kali na wasiwasi mkubwa matukio ya sasa huko Palestina.

Mapigano makali kati ya jeshi la Israel na raia wa Palestina, Quds

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu amesema kuwa, ukandamizaji unaofanywa sasa na Israel dhidi ya raia wa Palestina ni sehemu ya mikakati ya utawala huo ghasibu ya kuiyahudisha kikamilifu Quds tukufu. Amesema kuwa, Ulimwengu wa Kiislamu unakutambua kuvamiwa Msikiti wa al Aqsa na kituo alichotumia Mtume Muhammad (saw) kwa ajili ya safari yake ya mbinguni kuwa ni mstari wake mwekundu ambao haupaswi kuvukwa. 

Larijani amesisitiza kuwa, Bunge la Iran linapongeza mapambano halali ya watu wa Palestina kwa ajili ya kukomboa nchi na ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na linasisitiza juu ya udharura wa kuwajibika mabunge yote hususan mabunge ya nchi za Waislamu na jumuiya za kimataifa kwa shabaha ya kuzuia ukatili unaoendelea kufanywa na Israel.  

Jeshi la Israel likiwafyatulia risasi Waislamu kwenye viwanja vya Msikiti wa al Aqsa

Ijumaa ya tarehe 14 Julai Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliliamuru jeshi la utawala huo haramu kufunga milango yote ya kuingia katika Msikiti wa al Aqsa na kuwazuia Waislamu kutekeza ibada ya Swala msikitini hapo. Hatua hiyo imezusha ghasia na machafuko makubaa katika ardhi za Palestina na inaendelea kulaaniwa na nchi na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu.