Kim Yong-nam: Iran na Korea Kaskazini zina adui wa pamoja
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i32754-kim_yong_nam_iran_na_korea_kaskazini_zina_adui_wa_pamoja
Mkuu wa Kongresi ya Taifa ya Watu wa Korea Kaskazini Kim Yong-nam amepongeza taifa la Iran kwa msimamo wake imara na kusema kuwa, anaona fahari kutembelea nchi ambayo ina adui wa pamoja na Korea Kaskazini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2017 22:39 UTC
  • Kim Yong-nam: Iran na Korea Kaskazini zina adui wa pamoja

Mkuu wa Kongresi ya Taifa ya Watu wa Korea Kaskazini Kim Yong-nam amepongeza taifa la Iran kwa msimamo wake imara na kusema kuwa, anaona fahari kutembelea nchi ambayo ina adui wa pamoja na Korea Kaskazini.

Kim Yong-nam ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge), Ali Larijani na kusema: “Tangu awali Iran ilitangaza kuwa haitaruhusu kuunda silaha za nyuklia au kuanza kuishambulia nchi nyingine na sisi pia tunaunga mkono msimamo huo.” Kim Yong-nam,  amesema kuwa, licha ya muda kusonga mbele lakini Iran na Korea Kaskazini bado zimeendelea kuwa na adui wa pamoja na kwamba hadi sasa Marekani ingali inaendeleza siasa zake za kibeberu dhidi ya nchi hizo.

Kim Yong-nam kushoto alipozungumza na Ali Larijani

Kadhalika  mkuu wa Bunge la Watu wa Korea Kaskazini ametaka kuimarishwa zaidi mahusiano ya Tehran na Pyongyang hususan katika Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) na katika ngazi ya kimataifa kwani mahusiano hayo yana maslahi kwa watu wa mataifa hayo mawili. Amesisitiza kuwa, Korea Kaskazini inataka maendeleo lakini kamwe haitafumbia macho haki yake hata kidogo na kuongeza kuwa, madamu Marekani inaendeleza siasa zake za uchokozi na vitisho dhidi ya Pyongyang, basi Korea Kaskazini nayo itaendelea kujiimarisha zaidi kwa ajili ya kutoa jibu kali kwa uadui wake huo.

Kwa upande wake Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge), Ali Larijani, amesema kuwa, Iran inatetea miradi ya nyuklia ya amani lakini wakati huo huo inaamini kuwa, silaha za nyuklia za nchi yoyote zina madhara kwa usalama na amani ya dunia. Spika Larijani ameongeza kuwa, machafuko ya sasa duniani hayana maslahi kwa nchi yoyote na kinyume chake, yanadhuru pande zote na kwa sababu hiyo kuimarisha usalama na amani ya dunia ndio suala linalotakiwa kupewa umuhimu na nchi zote.

Kim Yong-nam alipokutana pia na Rais Hassan Rouhani wa Iran

Aidha Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amepongeza msimamo wa Korea Kaskazini dhidi ya mabeberu kwa kusema: “Tunapongeza msimamo wenu dhidi ya ubeberu wa Marekani na tunataraji kwamba, usalama na amani ya dunia vitapatikana haraka iwapo nchi zinazopenda kujitanua duniani zitaachana na mwenendo wao huo wa kuzisakama nchi nyingine”, mwisho wa kunukuu.