Brigedia Jenerali Hatami: Iran itaendelea kuunga mkono muqawama
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuunga mkono mhimili wa muqawama.
Brigedia Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Iran ameyasema hayo leo katika hafla ya kumtambulisha rasmi katika wizara hiyo ambapo sambamba na kutoa mkono wa pongezi kwa maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ulinzi amesema: Uungaji mkono wa pande zote wa Wizara ya Ulinzi kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Jeshi na Vikosi vya Polisi katika sekta za ulinzi wa anga, makombora, majini na nyenginezo zenye umuhimu utaendelea kwa nguvu zote.
Brigedia Jenerali Hatami ameongeza kuwa: Nguvu na uwezo ilionao Iran ya Kiislamu leo hii katika uga wa sekta ya ulinzi umepatikana kwa juhudi za wataalamu wa sekta hiyo, mawaziri wa ulinzi waliotangulia na wafanyakazi waaminifu wa Wizara ya Ulinzi.
Siku ya Jumapili, wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) walimpigia Brigedia Jenerali Amir Hatami kura 261 za kuwa na imani naye na kumuidhinisha kuwa Waziri wa Ulinzi wa serikali mpya ya Rais Hassan Rouhani. Inafaa kuashiria kuwa tarehe 22 Agosti kila mwaka huadhimishwa hapa nchini Iran kuwa Siku ya Sekta ya UIinzi.../