Sep 04, 2017 07:49 UTC
  • Iran yapinga ripoti ya Asma Jahangir Kuhusu Haki za Binadamu Nchini

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: ''Ripoti mpya ya Asma Jahangir, mkaguzi maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu Iran, imetolewa kwa malengo machafu ya kisiasa na ya kimapendeleo na hivyo Iran haikubali hata kidogo ripoti hiyo."

Akizungumza Jumapili, Bahram Qassemi ameongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa pamoja na kuwepo majibu ya mara kwa mara, marefu na yenye nyaraka na ushahidi ambayo yametolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kujibu madai yasiyo na msingi, ripoti za baraza hilo zingali zinategemea taarifa zisizo sahihi na kutoa hukumu bila kuchunguza hali ya haki za binadamu nchini Iran. Ripoti hizo zinategemea marejeo yasiyo na itibari na hivyo kutia dosari kubwa ripoti hiyo ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Suala la haki za binadamu limekuwa likitumiwa kama moja ya njia nyingine zinazotumiwa kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Madola ya Magharibi hutumia haki za binadamu kuzishinikiza nchi huru ambazo hazikubali kufuata kibubusa sera za madola hayo ya kibeberu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama nchi yenye misimamo huru na ya kujitegemea kwa muda mrefu imekuwa ikilengwa kwa kutofuata misingi ya haki za binadamu inayofuatwa na nchi za Magharibi.

Bahram Qassemi

Kwa kawaida wakaguzi maalumu wa  haki za binadamu dhidi ya Iran huteuliwa kwa malengo maalumu ya kuonyesha taswira isiyo sahihi ya haki za binadamu nchini. Kwa msingi huo wakaguzi hao hutegemea marejeo na taarifa zisizo sahihi na kuzifanya kuwa msingi wa ripoti zao za  hali ya haki za binadamu nchini.

Ayatullah Amoli Larijani, Mkuu wa Idara ya Mahakama Iran Jumatatu wiki aliyopita alisema: "Kile ambacho kinasemwa na mahasimu , makundi yaliyo dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kundi la kigaidi la munafikina dhidi ya Iran, hupatikana katika ripoti za mkaguzi maalumu wa Baraza la Haki za binadamu kuhusu Iran."

Marejeo yanayotumiwa na mkaguzi wa Baraza la Haki za Binadamu huwa na lengo maalumu la kuonyesha taswira potofu kuhusu hali halisi ya mambo Iran. Idara ya Mahakama katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hutegemea sheria zinazotokana na mafundisho ya Kiislamu katika suala la haki za binadamu. 

Kwa mfano, hukumu ya kunyongwa katika mahakama za Iran hutegemea mafundisho ya Kiislamu. Hali kadhalika kuhusu wanawake, Iran imewapa wanawake hadhi kubwa kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu na hivyo wana hali nzuri ya kijamii hata ikilinganishwa na nchi za Magharibi.

Kuhusu haki za waliowachache nchini Iran, Wamagharibi wenyewe wanakiri waliowachache wana  hali nzuri na ya kuridhisha nchini Iran.

Yonatan Betkolia  mjumbe wa wafuasi wa dini ya Ashuri (Assyrian) katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, anabainisha zaidi kwa kusema: "Wafuasi wa dini za waliowachache Iran wanapata haki sawa na Wairani wengine."

Kwa ujumla ni kuwa, muelekeo wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni muelekeo unaoegemea upande mmoja.  Mkaguzi maalumu wa baraza hilo hutoa ripoti zisizo sahihi kuhusu hali ya haki za binadamu Iran huku taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa ikifumbia macho ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa katika maeneo mengine duniani.

Umoja wa Mataifa umepuuza jinai zinazotekeelzwa na Saudia Yemen

Ni wachache duniani wasiojua kuhusu hali mbaya ya Haki za Binadamu nchini Saudi Arabia na katika utawala wa Kizayuni wa Israel na hivi sasa katika nchi ya Myanmar. Lakini Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa hutazama masuala hayo kisiasa na hivyo kudhoofisha itibari na hadhi yake.

Tunashuhudia namna Waislamu wa Yemen wanavyouawa kila siku kupitia silaha zilizopigwa marufuku zinazotumiwa na utawala wa Saudia na nchini Myanmar hivi sasa kunajiri mauaji ya kimbari ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Palestina nayo  kwa miongo sita imekuwa ikishuhudia ukatili usio na kifani wa utawala haramu wa Israel. Hiyo ni mifano michache tu ya ukiukwaji wa haki za binadamau unaopuuzwa na Umoja wa Mataifa. Kama alivyosema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, 'muelekeo huu wa undumakuwuli umepelekea kudhoofika itibari ya Baraza la Haki za Binadamu kimataifa na kwa hakika ni kashfa kubwa kwa wale wanaodai kutetea haki za binadamu duniani."

Tags