Iran: Jamii ya kimataifa ikomeshe mauaji ya Waislamu wa Myanmar
-
Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kivitendo za kukomesha uangamizaji wa kizazi wanayofanyiwa Waislamu wa kabila la Rohingya na mabudha wa Myanmar.
Mohammad Javad Zarif alisisitiza hayo jana katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Tweeter na kuongeza kuwa, hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya mauaji ya kimbari wanayofanyiwa Waislamu wa Rohingya.
Amesema, jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za haraka za kuwaokoa Waislamu wa Myanmar kabla ya kuchelewa zaidi.
Wimbi jipya la mauaji ya Waislamu nchini Myanmar hasa katika eneo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo limeshapelekea kuuawa Waislamu wasiopungua 400.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, karibu Waislamu laki moja na 64 elfu wamekimbilia nchi jirani ya Bangladesh katika kipindi kifupi cha wiki mbili tu kutokana na ukatili wa kuchupa mipaka wanaofanyiwa na mabudha. Serikali ya kibudha ya Myanmar inawanyima Waislamu wa nchi hiyo hata haki yao ya kimsingi kabisa yaani ya uraia.