Amano: Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu JCPOA
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa Iran imeheshimu na kutekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano ya nyuklia maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Yukia Amano alisema jana Jumatatu kuwa, wakala wa IAEA ulikuwa na nafasi kuu katika utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA na kufikiwa makubaliano ya nyuklia na akasisitiza kwa mara nyingine kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza majukumu yake kuhusiana na makubaliano hayo. Aidha ameongeza kuwa, majukumu yote ya kinyuklia ya Iran kuhusu JCPOA yametekelezwa.
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hadi kufikia sasa umethibitisha mara nane kwamba Iran imeheshimu na kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo ya nyuklia; huku Marekani iking'ang'ania kuwa Iran imekwenda kinyume na makubaliano hayo licha ya wakala wa IAEA kukagua mara kwa mara vituo vya nyuklia hapa nchini.