Iran: Wanawake ndio wahanga wakuu wa magenge ya kigaidi
(last modified Sat, 28 Oct 2017 08:06:02 GMT )
Oct 28, 2017 08:06 UTC
  • Iran: Wanawake ndio wahanga wakuu wa magenge ya kigaidi

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema wanawake ndio wahanga wakuu wa ukatili wa makundi ya kigaidi duniani.

Gholamali Khoshroo ameyasema hayo katika taarifa iliyotolewa jana Ijumaa, kabla ya kuanza Kikao cha Wazi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuhusu Wanawake, Amani na Usalama.

Amesema uingiliaji wa kijeshi wa baadhi ya nchi sanjari na nchi hizo kukalia kwa mabavu ardhi za nchi nyingine kumepelekea kushtadi harakati za magenge ya kigaidi na kitakfiri katika eneo la Mashariki ya Kati, na aghalabu wanawake na wasichana ndio wahanga wa jinai za makundi hayo. 

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema harakati hizo zimewafanya wanawake na wasichana wadogo kupoteza matumaini ya kuwa mustakabali mzuri.

Wanawake na watoto wadogo, wahanga wakuu wa ugaidi

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amefafanua kuwa: "Kwa masikitiko, katika migogoro mingi duniani hususan Mashariki ya Kati, wanawake wameendelea kuwa wahanga wakuu wa jinai zilizoratibiwa, hususan udhalilishaji wa kijinsia. Jinai zinazofanywa na magenge kama Daesh (ISIS), al-Shabaab na Boko Haram zimekuwa zikiwalenga na kuwaathiri zaidi wanawake na watoto wadogo."

 Gholamali Khoshroo amebainisha kuwa, kuna maelfu ya kesi za jinai za kingono dhidi ya wanawake, zinazotumiwa na magaidi kama silaha ya kivita katika nchi za Iraq, Syria, Somalia, Nigeria na Mali. 

 

Tags