Dec 12, 2017 03:00 UTC
  • Rouhani: Mataifa ya Kiislamu yatazima njama ya Marekani na Israel

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema umoja, muqawama na mapambano ya Wapalestina na nchi nyingine za Kiislamu bila shaka yatapelekea kusambaratika kwa njama ya Marekani na utawala wa Kizayuni ya kuitambua Quds tukufu kuwa 'mji mkuu' wa utawala haramu wa Israel.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake ya simu na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, Ismail Haniya.

Dakta Rouhani ameutaja uamuzi huo wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuutambua Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa Israel kuwa 'tusi'  kwa ulimwengu wa Kiislamu.

Rais wa Iran amemuambia kiongozi huyo mwandamizi wa harakati ya muqawama ya Hamas kuwa, na hapa tunanukuu: "Jamhuri ya Kiislamu inalaani vikali kitendo hicho cha Marekani. Hatua hiyo ghalati kwa mara nyingine tena imeweka wazi azma ya Marekani na Israel ya kutoheshimu haki za Wapalestina, licha ya kuwahadaa walimwengu kwamba zinataka 'suluhisho la Mashariki ya Kati'.

Wapalestina wakipambana na askari wa Israel huko Quds

Kwa upande wake, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas amesema kitendo hicho cha Trump ni ukiukaji wa wazi wa haki za Waislamu, huku akisisitiza kuwa, wananchi madhulumu wa Palestina katu hawatoiruhusu Marekani itekeleza mpango huo, kwani Quds tukufu ni ya Wapalestina na Waislamu wote kwa ujumla.

Kadhalika amesisitiza kuwa, wananchi wa Palestina watandeleza Intifadha mpya hadi wahakikishe kuwa njama hiyo Marekani na Wazayuni inasambaratika. 

Tags