Mshauri Mkuu wa Kiongozi Muadhamu: Marekani si dola kubwa tena duniani
Mshauri Mkuu wa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi Yote ya Iran amesema kuwa, kushindwa Marekani katika mpango wake wa kuitambulisha Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel kumeonesha kuwa, nchi hiyo si dola kubwa tena duniani.
Meja Jenerali Hassan Firuzabadi ambaye alikuwa akizungumza baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupasisha kwa kura nyingi azimio lililopinga hatua ya Marekani ya kuitambua Quds kuwa eti ni mji mkuu wa Israel amesema kuwa: Upinzani wa nchi 128 duniani dhidi ya mpango huo wa Marekani na jinsi nchi hizo zilivyotetea haki za Wapalestina ni tukio muhimu katika historia ya siasa ya dunia ambalo limeionesha tena Marekani kwamba sio dola kubwa duniani.
Vilevile Mshauri wa Amiri Jeshi Mkuu wa Iran ameashiria mchezo wa kuigiza na kuchekesha wa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley kuhusu kile alichodai ni misaada ya makombora ya Iran kwa wapiganaji wa Yemen ambayo yanatumiwa kupiga mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh na kusema: Nchi za Kiarabu za Mashariki ya Kati zinapaswa kushirikiana na nchi nyingine za eneo hili la kusitisha misimamo ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ya Saudi Arabia na Imarati.
Meja Jenerali Firuzabadi amesisitiza kuwa nchi hizo pia zinalazimika kukata uhusiano na Wazayuni na kurejea katika mikono ya Uislamu.