Qassemi: Iran daima inafanya juhudi za kutetea haki za taifa la Palestina
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya juhudi za kutumia mbinu za kidiplomasia kwa ajili ya kutetea haki za taifa la Palestina.
Bahram Qassemi amesema hayo leo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari wa ndani na nje na kubainisha kwamba, Iran itatumia mbinu zote kwa ajili ya kukabiliana na hatua isiyo ya kawaida ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitambua Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema bayana kwamba, Tehran siku zote imekuwa na unyeti maalumu na masuala muhimu kama kadhia ya Beitul-Muqaddas na katika mkutano wa hivi karibuni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mjini Istanbul Uturuki misimamo ya taifa hili ilitangazwa na kuwekwa wazi.
Bahram Qassemi amezungumzia kupasishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa azimio la kupinga hatua ya Rais Trump kuhusu Beitul-Muqaddas na kusema kwamba, tukio hilo limebainisha kutengwa Marekani na kubakia peke yake.
Amesema, viongozi wa Wamarekani wanapaswa kutambua kwamba, kwa kutumia mbinu hizo hawawezi kufikia malengo yao na kutaka jambo lao lifuatwe na wengine.
Aidha Bahram Qassemi amezungumzia makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mapango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kuzitahadharisha nchi za Ulaya zisije zikahadaika na hila na uafiriti wa Marekani.