Utambulisho Halisi wa Marekani kwa Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei Jumatano asubuhi katika mkutano na maafisa na wanachama wa Baraza la Kuhubiri Uislamu kutoka kote Iran aliashiria njama zisizo na kikomo za Marekani za kuvuruga na kuondoa matumaini katika taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa, 'Kwa msaada wake Mwenyezi Mungu na kwa kutegemea mwamko na kusimama kidete wananchi- sawa na huko nyuma- tutampa adui pigo. Kuwepo jitihada maradufu za wakuu wa nchi katika kutatua matatizo ya kimaisha na kiuchumi, tutaendelea na mkondo wetu wa ustawi kwa nguvu."
Utambulisho wa kiistikbari wa Marekani umelithibitikia taifa la Iran mara kadhaa. Lakini hakuna shaka kuwa, kile ambacho Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alichokisema kuhusu utambulisho halisi wa Marekani kinapaswa kutazamwa kama tahadhari kuhusu malengo ya kishetani ya Marekani katika eneo.
Hapa tunaweza kuangazia nukta kadhaa katika hotuba ya Kiongozi Muadhamu ambayo ilikumbusha kuhusu mpango wa muda mrefu wa Marekani katika eneo.
Nukta ya kwanza; Ukweli ni kuwa, Marekani, kinyume na madai yake ya kidhahiri, haina nia wala irada ya kuangamiza ugaidi katika eneo. Marekani kwa kuunga mkono ISIS au Daesh na magaidi wengine wakufurishaji na kushirikiana na tawala dhalimu na za kidikteta kama vile utawala wa Aal Saudi na pia kuunga mkono jinai za Wazayuni na umwagaji damu ya Wayeman kila siku ni mambo yanayoashiria utambulisho mchafu na fasidi wa Marekani.
Nukta ya pili; Marekani daima imekuwa ikipinga kuona nchi za Kiislamu zikiwa na nguvu na hasa inaupinga mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sababu ni mfano wa kuigwa katika kupinga ubeberu.
Nukta ya tatu; Kuna umuhimu wa kuendelea ustawi na si katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu tu bali katika nchi zote zinazojitegemea.
Lengo kuu la Marekani ni kuzishughulisha nchi za eneo na migogoro bandia kwa kuibua mifarakano na hitilafu za ndani ambazo wakati mmoja huchukua muundo wa kikabila na wakati mwingine kuibua fitina na kupindua serikali.
Kwa msingi huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake ameashiria kuhusu jitihada zisizo na kikomo za Marekani za kuvuruga na kuondoa matumaini na imani katika taifa la Iran na kusema: "Tarehe Tisa Dei na adhama yake ni siku ya taifa la Iran kutoa jibu kwa njama hizo na kulinda thamani za Mapinduzi ya Kiislamu na dini."
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kimsingi ilikuwa ni ufafanuzi wa malengo na njama za Marekani kieneo na kimataifa. Njama hizo za Marekani ndizo chanzo cha matatizo na masaibu ya mataifa ya eneo na dunia.
Noam Chomsky, mwananadharia mashuhuri wa Marekani katika kukosoa matamshi ya wakuu wa Marekani anasema hivi: "Marekani inaitaja Iran kuwa ni tishio kubwa zaidi la amani katika hali ambayo dunia inaamini kuwa Marekani ndiyo tishio kubwa kwa usalama wa dunia."
Marekani imeanzisha vita vingi vya dunia na pia ni chanzo cha migogoro mingi mbali na kutekeleza njama za kuangusha serikali halali kama ilivyofanya nchini Iran Agosti mwaka 1953.
Uungaji mkono wa makundi ya kigaidi kama ISIS ni kati ya vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na Marekani, lakini pamoja na hayo inadai kuwa eti Iran inavuruga uthabiti wa eneo.
Hakuna shaka kuwa, kama alivyosema Kiongozi Muadhamu, gharama kubwa na mipango mikuu ya Marekani kuibua hitilafu za kisiasa, kidini, kikaumu na kilugha nchini Iran hazijakuwa na faida na Washington imefeli katika njama hizo.
Kile ambacho kimeshuhudiwa ni kinyume walichokitarjajia Wamarekani, nacho ni ustawi wa Iran na mkondo huo utaendelea hata katika urais wa sasa wa Marekani. Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kupiga hatua za kimaendeleo kwa nguvu zake zote na kusisitiza kuwa: Njia hiyo ya maendeleo itaendelea pia katika kipindi cha rais wa hivi sasa wa Marekani na daima wataendelea kuwa na kinyongo cha kushindwa kuitoa Jamhuri ya Kiislamu katika medani au kuidhoofisha.