Bahram Qassemi: Wananchi wa Iran hawatishiki na makelele ya viongozi wa Marekani
Katika radiamali kwa matamshi ya uingiliaji wa viongozi wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, raia wa taifa hili hawatilii umuhimu nara za utumiaji fursa wa kupenda kujionyesha za viongozi wa Marekani.
Katika siku za hivi karibuni ambapo vyombo vya habari vya nchi hii vimekuwa vikikosoa siasa za Rais Donald Trump wa Marekani, rais huyo ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter akiitaka serikali ya Iran eti iheshimu haki za wananchi. Sambamba na kukosoa matamshi hayo ya kijuba ya Trump, Bahram Qassemi ameyataja kuwa yasiyo na itibari yoyote na kwamba, raia wa Iran wanafahamu vyema nafasi ya Trump katika kukiuka haki za binaadamu za raia madhlum wa Palestina, Yemen na Bahrain na kadhalika ushiriki wake katika miamala ya uhasama na chuki dhidi ya Wairani kwa kuwazuia kuingia Marekani sambamba na kuwakamata wale wanaoishi nchini humo kwa tuhuma tofauti.
Bahram Qassemi ameongeza kuwa raia wa Iran wanaufahamu utumiaji fursa na kujionyesha kwa viongozi wa Marekani kutokana na baadhi ya mikusanyiko ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika siku za hivi karibuni katika baadhi ya miji Iran kuwa si kitu kingine ghairi ya kujionyesha kwa serikali ya Washington. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kubainisha kwamba raia wa Iran ni wawasimamizi wakubwa wa usalama na maendeleo ya nchi, amesema kuwa, ushiriki wa Wairani katika chaguzi kwa ajili ya kuainisha mustakbali wao na kadhalika ushiriki wao wenye taathira katika asasi za kitaifa sambamba na ukosoaji wao kwa vyombo vya serikali, ni mambo yanayodhamini ustawi na kulinda mapinduzi yao ya Kiislamu.
Aidha amefafanua kuwa, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitabiri muundo wa kidemokrasia kwa ajili ya kuunga mkono kisheria matakwa ya kiraia ya wananchi na uwezekano wa kutatuliwa matatizo hayo katika kalibu ya sheria kamili.