Madai ya ovyo ya Marekani na kuzidi kuchanganyikiwa White House
Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, serikali ya Donald Trump nchini Marekani imeongeza uadui wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Chokochoko za karibuni kabisa za Ikulu ya Marekani, White House ni kitendo cha Trump cha kuwaalika chakula cha mchana mabalozi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuwaonesha kipande cha chuma ambacho Marekani inadai eti ni mabaki ya kombora la Iran lililovurumishwa nchini Saudi Arabia na Answarullah ya Yemen.
Nikki Haley, mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine ameendesha kampeni za kuthibitisha chuki za nchi yake kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwaonesha mabalozi wa nchi hizo kipande hicho cha chuma na kurudia madai kwamba eti ni kipande cha kombora la Iran. Kabla ya hapo Nikki Haley aliwahi kujitokeza mbele ya waandishi wa habari mjini Washington akiwa na kipande cha chuma na kudai kuwa ni sehemu ya kombora ambalo lilivurumishwa katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh na Mahuthi wa Yemen na kwamba eti kombora hilo lilotoka Iran hivyo akaituhumu Tehran kuwa inakiuka sheria za kimataifa.
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu tamthilia hiyo ya kisiasa ya Marekani na kuandika katika ukurasa wake wa Twitter ambapo maana yake ya kiujumla inasema, ...ilibidi hawa watu wawe wamefahamishwa kuwa kombora lililotunguliwa na kuangamizwa na makombora ya patriot angani halitui salama usalamini ardhini. Hata hivyo hivi sasa wamezuka na vipande vya kombora tena likiwa na muhuri wa viwango vya bidhaa za Iran ambao kwa hakika hautumiwi isipokuwa tu kwa ajili ya kuonesha viwango vya chakula, (si silaha). Hapo hapo akawaambia Wamarekani kwamba, hata katika kusema uongo pia, kunataka utaalamu hivyo wajaribu kutafuta uongo mwingine wa kueneza, si huu.
Marekani inaendesha siasa za pande tatu dhidi ya Iran. Upande wa kwanza ni kujaribu kuonesha kuwa uwezo wa makombora wa Iran ni tishio na kwamba kukabiliana na uwezo huo kuna umuhimu wa kiistratijia kwa Marekani. Upande wa pili ni kudai kuwa Iran eti inaunga mkono ugaidi na tatu ni madai ya kuvunjwa haki za binadamu. Yote hayo yanafanyika ili kuiweka chini ya mashinikizo Iran. Hivi sasa Donald Trump anadai kuwa mapatano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA ni maafikiano mabaya mno kuwahi kuyaona ili kwa madai hayo apate fursa ya kudhihirisha chuki zake dhidi ya Iran. Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, lengo la hatua ya Marekani ya kuwaalika dhifa ya chakula cha mchana, mabalozi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huko Washington ni kuyashinikiza mataifa ya dunia ili Washington ipate upenyo wa kuyatumia vibaya mapatano ya JCPOA.
Baada ya dhifa hiyo ya chakula cha mchana, Nikki Haley alidai kuwa msimamo wa jamii ya kimataifa dhidi ya mradi wa makombora ya balestiki ya Iran huenda ukamfanya Donald Trump akubali kubakia kwenye mapatano ya JCPOA.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hata wale watu wenye chuki na Iran huko Marekani kama vile Richard Lugar, mkuu wa zamani wa kamati ya uhusiano wa nje ya baraza la Senate la Marekani, au Paul O'Neill, waziri wa zamani wa hazina wa wakati wa urais wa George W. Bush, Michael Hayden, mkuu wa zamani wa Wakala wa Usalama wa Taifa na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA pamoja na Eric Olson, mkuu wa zamani wa vikosi maalumu vya Marekani; wote wamemtahadharisha Trump kwa kumwambia: "Siasa za Marekani kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA zinapaswa kusimama kwa mujibu wa manufaa ya usalama wa taifa wa Marekani na si kwa kutegemea hitilafu ndogo ndogo za kiaidiolojia."
Weledi wa Mambo wanasema kuwa, vitendo hivyo vya Marekani vyote vinalenga kwenye shabaha moja nayo ni kujaribu kuidhoofisha Iran katika chanjaa mbili za kiulinzi na kiuchumi na kujaribu kuitenga na kuiweka mbali katika masuala ya kieneo na kimataifa.
Hata hivyo, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwahi kuwaambia mamia ya vijana wenye vipaji na vipawa mbalimbali vya kielimu kwamba uadui wa Marekani kwa taifa la Iran ulianza zamani sana. Tangu katika siku za awali za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Alisema: Wakati huo hakukuwa na suala la nyuklia wala makombora na wala ushawishi wa kieneo wa Iran, lakini pamoja na hayo Wamarekani walikuwa wameshajua kwamba kutokana na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Washington imeipoteza Iran yenye manufaa mengi na haitokuwa tena nchi inayoitii Marekani.