Miamala ya kinafiki ya Marekani na kuwa macho wananchi wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39811-miamala_ya_kinafiki_ya_marekani_na_kuwa_macho_wananchi_wa_iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewahutubu viongozi wa Marekani akiwaambia kwamba, madai yao ya kuwaunga mkono wananchi wa Iran ni sawa na machozi ya mamba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 02, 2018 04:50 UTC
  • Miamala ya kinafiki ya Marekani na kuwa macho wananchi wa Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewahutubu viongozi wa Marekani akiwaambia kwamba, madai yao ya kuwaunga mkono wananchi wa Iran ni sawa na machozi ya mamba.

Rais Rouhani amesisitiza akiwaambia viongozi wa Marekani kwamba: Wananchi wa Iran hawajasahau uvamizi wenu Mashariki ya Kati; nyinyi ndio mlioivamia kijeshi Afghanistan na baadaye Iraq, nyinyi ndio mnaolisaidia kundi la kigaidi la Daesh na nyinyi ndio ambao hamtaki kuona eneo la Mashariki ya Kati linashuhudia amani na usalama.

Rais Rouhani alisema hayo jana Alkhamisi akiwa Sirjan, mkoani Kerman kusini mashariki mwa nchi katika siku ya kwanza ya maadhimisho ya Alfajiri Kumi za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, mtu asidhani kwamba, anaweza kulichukulia maamuzi taifa la Iran akiwa huko Washington.

Amesema akiwaambia viongozi wa Marekani: Wananchi wa Iran wameona jinai zenu katika kipindi chote cha historia na hawajaisahau idara ya usalama ya SAVAK ya kipindi cha utawala wa Shah pamoja na mateso ya kinyama ya Savak yaliyoasisiwa na nyinyi

Rais Donald Trump wa Marekani

Rais Rouhani amesema bayana kwamba, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu daima wananchi wa Iran wamekuwa wakijitolea; na kila mara Iran inapopata tatizo, wananchi hawa hujitokeza uwanjani na kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

Taashira ya Rais Rouhani kwa miamala ya chuki na hasama ya viongozi wa Marekani dhidi ya taifa la Iran inahusiana na uungaji mkono wao kwa wafanya fujo za hivi karibuni katika miji kadhaa ya Iran katika hali ambayo, Septemba mwaka jana ni viongozi hao hao Marekani ambao waliwaita wananchi wa Iran kwamba ni magaidi.

Aina hii ya muamala wa kinafiki wa viongozi wa Marekani kwa taifa la Iran imeshuhudiwa mara nyingi katika kipindi cha miaka 40 iliyopita cha Mapinduzi ya Kiislamu.

Hata katika zama za kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kitendo cha kufanya mapinduzi dhidi ya serikali halali ya Waziri Mkuu Mohammad Mosaddegh ni ishara ya wazi ya muamala wa kinafiki wa Marekani kwa taifa la Iran ambao kidhahiri unaonekana kuwa muamala wa kirafiki.

Makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA)

Baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, muamala wa kinafiki wa Marekani ulishika kasi na kuchukua mkondo mpana zaidi, na serikali mbalimbali zilizoingia madarakani nchini Marekani iwe ni Wademokrats au Warepublican waliliwekea vikwazo taifa la Iran mara elfu kwa visingizo mbalimbali. Wakati mwingine kwa madai ya haki za binadamu na kipindi fulani kwa tuhuma za kuunga mkono ugaidi katika Mashariki ya Kati.

Katika fremu hii, Marekani ililiwekea vikwazo taifa la Iran hata katika sekta ya dawa ambayo ni huduma muhimu, dola ambalo siku zote limekuwa likipiga ngoma ya kutetea haki za binadamu. Tukipekua kurasa za historia ya Mapinduzi ya Kiislamu tunashuhudia dhahiri shahiri chuki na uadui mkubwa uliofanywa na Marekani dhidi ya wananchi wa taifa hili pamoja na mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini.

Kwa muktadha huo, nara za Marekani kwamba, ni rafiki wa wananchi wa Iran ni hadaa na ghiliba ya wazi. Kutunguliwa ndege ya abiria ya Iran na jeshi la Marekani na kupelekea kuuawa abiria wote waliokuwamo ndani ya ndege hiyo ni ushahidi mwingine wa uadui wa wazi na wa moja kwa moja wa Marekani dhidi ya Iran.

Aidha kutumia Rais Donald Trump jina bandia badala ya kutumia lile la asili la Ghuba ya Uajemi ni ishara ya wazi ya uadui alionao Rais wa sasa wa Marekani dhidi ya taifa hili. Vile vile katika suala la makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) uadui wa Wamarekani dhidi ya taifa hili umefikia kileleni.

Hatua ya Marekani ya kuliwekea vikwazo tofauti taifa la Iran licha ya Washington kutia saini makubaliano hayo ya nyuklia kwa mara nyingine tena imewathibitishia wananchi wa Iran na walimwengu kwa ujumla kwamba, Wamarekani si watu wa kuaminika.

Miamala yote hiyo inathibitisha jambo moja tu nalo ni uadui mkubwa na wa daima wa Marekani dhidi ya mfumo wa Jamhuri yya Kiislamu ya Iran, ambao hii leo umekuwa ukifanya mambo katika nyuga zote kwa kujitegemea na kutokubali kuburuzwa, kinyume kabisa na irada na matakwa ya Marekani.