Zarif: Kushindwa Daesh (ISIS) si mwisho wa ukufurishaji duniani
Waziri wa Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kusambaratishwa kundi la kigaidi na la wakufurishaji la Daesh (ISIS) sio mwisho wa harakati za magenge ya ukufurishaji yenye misimamo ya kufurutu ada katika eneo hili.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo wakati alipohutubia Mkutano wa Usalama wa Munich (MSC) nchini Ujerumani na kuongeza kuwa, kushindwa kwa moja ya megenge hatari zaidi duniani hakumaanishi kuwa hatari ya misimamo mikali ya kuchupa mipaka imeondoka katika eneo hili la Mashariki ya Kati na kote duniani.
Dakta Zarif ametahadharisha kuwa, iwapo mizizi ya ukufurishaji haitang'olewa, basi yumkini aidiolojia ya chuki na uhasama ya makundi yenye misimamo mikali itaibuka katika maeneo mengine ya dunia.
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, Marekani na vibaraka wake katika eneo hili kwa sasa mambo ya yanawaendea kombo kutokana na maamuzi mabaya waliyoyachukua huko nyuma.
Amesema ni jambo la kushangaza kuona Marekani na waitifaki wake wanailekezea kidole cha lawama Iran, katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu imekuwa katika upande mzuri wa historia kwa kukabiliana na Dikteta Saddam Hussein, makundi ya kigaidi ya al-Qaeda, Taliban, ISIS, Jabhatun Nusra na mfano wake.
Kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran, Dakta Javad Zarif amesema, mapatano hayo ni mfano wa kuigwa wa kuupatia ufumbuzi mgogoro, kwa kuzingatia tofauti zilizopo kwa shabaha ya kufikia lengo moja, na kwa kuheshimu maslahi ya pande zote husika.
Wakati huo huo, Dakta Zarif ameyataja matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu katika kikao hicho kama mchezo wa kuigeiza wa katuni, ambayo hayana hata hadhi ya kujibiwa.
Huku akiwa amebeba kile alichokitaja kama pande la mabaki ya ndege isiyo na rubani ya Iran aliyodai eti imetunguliwa na jeshi la Israel zaidi ya wiki moja iliyopita, Netanyahu amedai kuwa Tel Aviv ina uwezo wa kutoa jibu la moja kwa moja dhidi ya Iran.