Iran: Marekani inawasaidia wavamizi wa Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40931-iran_marekani_inawasaidia_wavamizi_wa_yemen
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, madai ya kukaririwa na ya kuchosha ya mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa dhidi Iran ni msaada kwa wavamizi wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2018 04:27 UTC
  • Iran: Marekani inawasaidia wavamizi wa Yemen

Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, madai ya kukaririwa na ya kuchosha ya mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa dhidi Iran ni msaada kwa wavamizi wa Yemen.

Taarifa iliyotolewa na mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa imesema kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekadhibisha mara kwa mara madai ya Marekani kuwa Tehran inatuma silaha nchini Yemen na inasisitiza tena kwamba, mashambulizi ya mabomu ya miaka mitatu dhidi ya Yemen yamesababisha maafa makubwa. 

Taarifa hiyo imesema kuwa, watoto, wanawake na watu wa Yemen kwa ujumla wanasumbuliwa na maradhi, njaa na vita na kwamba mashambulizi yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen kwa kutumia silaha za Marekani na Uingereza yamevuruga usalama na amani.

Taarifa ya balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, tatizo la Yemen haliwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi na mashambulizi ya mabomu bali Iran inaamini kuwa, kusitishwa mashambulizi na kupeleka misaada ya chakula na maji kwa raia wa nchi hiyo kunaweza kufungua njia ya mchakato wa kisiasa kwa ajili ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo. 

Saudia yaendelea kuua raia wa Yemen

Taarifa ya ofisi ya mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa imesisitiza kuwa, hatua ya mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa imechukuliwa kwa ajili ya kuficha na kufunika jinai na uhalifu unaofanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen.

Marekani na Uingereza jana zilitaka kutumia vibaya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuwasilisha muswada uliotuhumu Jamhuri ya Kiislamu kuwa inatuma silaha nchini Yemen. 

Muswada huo uliopendekezwa na Uingereza kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, umekwamishwa na kura ya veto ya Russia.