Larijani: Suala la makombora ya Iran halijadiliki
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa nchi za Ulaya hazipasi kuunganisha kadhia ya makombora ya Iran na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA bali zinapasa kushughulikia majukumu yao na ya Marekani kuhusu makubaliano hayo.
Akizungumza jana Jumamosi hapa Tehran na Yusuf bin Alawi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman aliyeko ziarani hapa nchini, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa suala la makombora ya Iran limezitia dukuduku baadhi ya nchi na kwamba Iran inamiliki teknolojia ya makombora tangu miaka 30 iliyopita na si jambo jipya. Ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kurusha makombora dhidi ya nchi nyingine.
Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa Iran imetekeleza majukumu yake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia na kwamba itaendelea kutekeleza majukumu yake maadamu pande nyingine zinatekeleza majukumu yao.
Ali Larijani amesema kuwa nafasi ya Oman na Sultan Qaboos katika eneo hili na Mashariki ya Kati siku zote imekuwa ya manufaa na yenye taathira zaidi na siku zote kumekuwepo uhusiano wa kirafiki na wa kuaminiana kati ya Iran na Oman.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yusuf bin Alawi amesema katika mazungumzo hayo kuwa: Baadhi ya nchi zina wasiwasi na siasa za kiulinzi na za makombora za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hata hivyo hakuna sababu yoyote ya kuwa na hofu kwa sababu hali ya mgogoro iliyoko katika eneo hili inaipa haki Iran kumiliki nguvu za kijeshi kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi yake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ameongeza kuwa zipo nyanja nzuri za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Iran na Oman na kiwango cha uhusiano huu kinapasa kuzidishwa sawa kabisa na uhusiano wa kisiasa.