Iran na Oman zasisitizia ulazima wa kuimarishwa amani na uthabiti katika eneo
Rais Hassan Rouhani amesisitiza juu ya kuimarishwa na kustawishwa zaidi uhusiano uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman.
Rais Rouhani ametoa sisitizo hilo leo hapa mjini Tehran katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yusuf bin Alawi.
Amesema kuna umuhimu wa kustawishwa uhusiano wa kibenki na kurahisisha utoaji suhula kwa wafanyabiashara wa nchi mbili kwa ajili ya kupanua ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi wa pande mbili na akasisitiza kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kwa dhati kustawisha katika pande zote uhusiano na ushirikiano wake na Oman.
Sambamba na kuashiria kwamba leo hii Iran na Oman zina jukumu zito kuhusiana na masuala ya eneo na inapasa zitumie tajiriba na uzoefu wao kwa ajili ya kuimarisha amani na uthabiti wa eneo, Dakta Rouhani amesema: kadiri amani na uthabiti unavyozidi kuvurugika katika eneo ndivyo nchi za eneo hili zinavyopata hasara zaidi.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia pia udharura wa kufanywa juhudi za kuhitimishwa mashambulio na mauaji ya raia wa Yemen na kuongeza kuwa, ana matumaini kwamba ushirikiano baina ya pande mbili za Iran na Oman utaweza kuwasaidia wananchi wa Yemen na kupelekea kurejeshwa amani na utulivu nchini humo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ameashiria uhusiano na ushirikiano wa kirafiki wa nchi mbili ambao umezidi kuimarika katika miaka ya karibuni na kueleza kwamba: Oman siku zote imekuwa ikitaka kuwa na uhusiano wa pande zote na wa kiwango cha juu kabisa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na inafanya juhudi za kupanua ushirikiano wake wa kibiashara na kiutamaduni na Tehran.
Yusuf bin Alawi amesifu pia umuhimu na uzito ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikilipa suala la kuimarisha amani na uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kwamba: mapigano nchini Yemen hayajawa na tija nyingine kwa eneo zaidi ya kusababisha masaibu na kuvurugika hali ya mambo. Bin Alawi amesema inapasa zifanyike jitihada kuhakikisha mauaji ya raia nchini humo yanakomeshwa haraka iwezekanavyo na misaada ya kibinadamu inawafikia raia hao.../