Zimbabwe yataka kuimarisha zaidi uhusiano wake na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i42688-zimbabwe_yataka_kuimarisha_zaidi_uhusiano_wake_na_iran
Makamu wa Rais wa Zimbabwe amehimiza kuimarishwa uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 05, 2018 10:14 UTC
  • Zimbabwe yataka kuimarisha zaidi uhusiano wake na Iran

Makamu wa Rais wa Zimbabwe amehimiza kuimarishwa uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo leo na kuongeza kuwa, Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Constantino Guveya Dominic Nyikadzino Chiwenga amesema hayo alipoonana na balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Harare na huku akikumbushia uhusiano wa muda mrefu wa Zimbabwe na Iran amesema kuwa, nchi yake ina hamu ya kuona uhusiano wake na Iran unaimarika katika nyuga tofauti.

Chiwenga ameongeza kuwa, kuna nyuga nyingi za kuimarisha uhusiano wa Tehran na Harare na zaidi ushirikiano wa kibiashara ambapo amesema, sekta binafsi zina jukumu la kuhakikisha ushirikiano wa kibiashara wa nchi mbili unaimarika.

Bendera za Iran na Zimbabwe

 

Kwa upande wake, Ahmad Erfanian, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Zimbabwe ameelezea kufurahishwa kwake na makabidhiano ya madaraka yaliyofanyika kwa njia ya amani huko Zimbabwe na kuzungumzia uhusiano wa kirafiki wa nchi hizi mbili akisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano wake na Zimbabwe kutokana na fursa mpya zilizojitokeza nchini humo.

Itakumbukuwa kuwa,  Emmerson Dambudzo Mnangagwa aliapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe tarehe 24 Novemba 2017 kuchukua nafasi ya Robert Gabriel Mugabe aliyelazimishwa kujiuzulu na jeshi na chama chake cha Zanu-PF.