Zarif aimbia NAM; Israel ndiyo tishio kuu kwa usalama wa dunia
Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel ndilo tishio kubwa zaidi kwa usalama wa dunia huku akitoa mwito wa kuanzishwa uchunguzi wa kimataifa juu ya jinai za utawala huo dhidi ya Wapalestina.
Akihutubu leo Alkhamisi katika mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) katika mji mkuu wa Azerbaijan, Baku, Mohammad Javad Zarif sambamba na kulaani hatua ya vikosi vya usalama vya Israel ya kuwaua na kuwajeruhi mamia ya Wapalestina wa Ghaza, amesisitiza kuwa kuna udharura wa kuanzishwa uchunguzi mara moja juu ya ukatili huo.
Dakta Zarif amesema, "Tunapaswa kulaani mauaji dhidi ya raia wa Palestina, wakiwemo wanawake na watoto wadogo. Tunataka uchunguzi wa kimataifa uanzishwe ili kuhakikisha kuwa haki za Wapalestina zinalindwa, sambamba na kuhitimishwa kughusubiwa ardhi zao."
Itakumbukwa kuwa siku ya Ijumaa wanajeshi wa utawala katili wa Israel waliwafyatulia risasi za kivita na kuwaua shahidi Wapalestina 18 na kujeruhi mamia ya wengine wakati wa maandamano ya amani ya kutetea haki ya wakimbizi Wapalestina kurejea katika ardhi zao zilizoporwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Iran ametaka kuhuishwa jitihada za kuundwa taifa huru la Palestina, mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu, sambamba na kuondolewa mzingiro wa kibaguzi dhidi ya Wapalestinawa Ukanda wa Ghaza.
Mkutano wa ngazi ya mawaziri wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) mefunguliwa leo Alkhamisi, kwa kuwaleta pamoja wawakilishi 800 kutoka nchi wanachama 120, nchi 17 wanachama watazamaji, pamoja na asasi 10 za kimataifa, chini ya kaulimbiu "Kuunga mkono amani na usalama wa kimataifa, kwa ajili ya maendeleo-endelevu".