Amano asisitiza tena kuwa Iran imeshikamana kikamilifu na mapatano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45424-amano_asisitiza_tena_kuwa_iran_imeshikamana_kikamilifu_na_mapatano_ya_jcpoa
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya karibuni kabisa ya wakala huo, Iran imeshikamana kikamilifu na mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2018 22:37 UTC
  • Amano asisitiza tena kuwa Iran imeshikamana kikamilifu na mapatano ya JCPOA

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya karibuni kabisa ya wakala huo, Iran imeshikamana kikamilifu na mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Yukiya Amano alisema hayo katika taarifa yake ya jana Jumatatu kwenye kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kuongeza kuwa, wakala huo unatekeleza vizuri protokali ya ziada ambayo inauruhusu kukagua maeneo na taasisi zote za Iran ambazo unahisi kuna udharura wa kukaguliwa na kwamba Iran haiwawekei kizuizi chochote maafisa wa IAEA.

Amesisitiza kuwa, ushirikiano mzuri na wa kina wa Iran katika kufungua milango ya kufaya ukaguzi huo umeirahisishia IAEA kufanya vizuri kazi zake ikiwa ni pamoja na kutekeleza ipasavyo protokali ya ziada.

Yukiya Amano (kushoto) akisalimiana na Rais Hassan Rouhani wa Iran mjini Tehran

 

Taarifa ya Amano imeongeza kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa ombi la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwa mujibu wa uwezo iliopewa IAEA na Bodi ya Magavana ya wakala huo, inaendelea vizuri kufanya ukaguzi na kusimamia utekelezaji wa Iran wa vipengee vya mapatano ya JCPOA.

Hadi hivi sasa wakala wa IAEA umeshatoa ripoti mara 11 na mara zote umesisitiza kuwa Iran imeshikamana kikamilifu na mapatano hayo ya nyuklia yaliyofikiwa mwaka 2015 baina ya Iran na kundi la 5+1.

Tarehe 8 Mei mwaka huu, Marekani ilidhihirisha utovu wake wa uaminifu kwa kutangaza kujitoa katika mapatano hayo licha ya kwamba ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha.