Qassemi: Jinai ya Marekani ya kutungua ndege ya abiria ya Iran haitasahaulika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46538-qassemi_jinai_ya_marekani_ya_kutungua_ndege_ya_abiria_ya_iran_haitasahaulika
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa Wairani kamwe hawatasahau jinai ya shambulizi la meli ya kivita ya Marekani dhidi ya ndege ya abiria ya Iran katika anga ya maji ya Ghuba ya Uajemi.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 03, 2018 10:52 UTC
  • Qassemi: Jinai ya Marekani ya kutungua ndege ya abiria ya Iran haitasahaulika

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa Wairani kamwe hawatasahau jinai ya shambulizi la meli ya kivita ya Marekani dhidi ya ndege ya abiria ya Iran katika anga ya maji ya Ghuba ya Uajemi.

Bahram Qassemi amesema kuwa, shambulizi la manoari ya Marekani dhidi ya ndege ya abiria ya Iran miaka 30 iliyopita ni doa la fedheha katika kipaji cha uso wa Marekani ambayo haisiti kukiuka na kukanyaga sheria na kanuni za kimataifa. Amesema Marekani si tu kwamba haikuonesha masikitiko ya aina yoyote baada ya kutenda jinai na mauaji hayo bali pia ilimtunuku nishani ya ushujaa kamanda wa manuari hiyo ya kivita kwa kuua mamia ya raia wasio na hatia yoyote!

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, uchunguzi wa mienendo ya Marekani kuhusu taifa la Iran na mataifa mengine unaonesha kuwa, nchi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kutenda unyama na ukatili dhidi ya binadamu kwa shabaha ya kupata maslahi na kutimiza malengo yake maovu; na haki za binadamu kwa Wamarekani ni kisingizio kinachotumiwa kwa malengo ya kujipanua na kutimiza maslahi haramu.

Itakumbukwa kuwa tarehe 3 Julai miaka 30 iliyopita manowari ya jeshi la Marekani, USS Vincennes ilifyatua makombora mawili dhidi ya ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege ya Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, na kuua shahidi watu wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo. Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama wa serikali ya Marekani.