Iran yamlaani Trump kwa amri yake yenye kuitusi OPEC
Iran imesema Rais Donald Trump wa Marekani ameitusi Jumuiya ya Nchi Zinazouza Mafuta ya Petroli kwa Wingi Duniani OPEC, kwa kuiamuru iongeze uzalishaji na ipunguze bei.
Waziri wa Mafuta wa Iran Bijan Zanganeh amesema msingi wa OPEC ni kuwa soko la mafuta ghafi ya petroli halipaswi kuwa la kisiasa na masuala ya kisiasa hayapaswi kutumiwa kuingilia soko ili lenyewe liainishe bei kwa mujibu wa taratibu za kibiashara.
Amesema baadhi ya hatua za kisiasa na ukosefu wa uthabiti huibua wasiwasi katika soko la mafuta na kupelekea kuongezeka bei na mfano wa hilo ni amri hiyo ya Trump ambayo ni tusi kwa mamlaka ya kujitawala ya nchi za OPEC.
Zanganeh pia amesema matamshi ya Trump yamepelekea bei ya mafuta duniani kuongezeka katika siku za hivi karibuni. Amesema amri ya Trump ni tusi kwa wananchi wa nchi za OPEC.
Siku ya Jumatano Trump alizituhumu nchi za OPEC kuwa zinapelekea bei ya mafuta kuongezeka huku akiamuru waitifaki wa Marekani katika shirika hilo, hasa Saudi Arabia, wazalishe mafuta mengi zaidi iwapo wanataka Washington iendelee kuwasaidia kukabiliana na Iran.