Iran yajenga kiwanda kipya cha rafadha za mashinepewa
Iran imekamilisha ujenzi wa kiwanda kipya cha kisasa cha kuunda rafadha za mashinepewa ili kuimarisha urutubishaji madini ya urani pasina kukiuka mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Ali Akbar Salehi Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran ameliambia Shirika la Habari la IRIB kuwa mradi huo umeanza kazi kufuatia dikrii ya hivi karibuni ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliyetaka uwezo wa kurutubisha urani nchini ufike SWU 190,000.
Salehi amesema Iran imekuwa ikijenga kiwanda hicho katika kipindi cha mazungumzo ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na madola makubwa duniani mwaka 2015. Amesema kiwanda hicho kipya kinaweza kuunda rafadha 60 za mashinepewa aina ya IR-6 kila siku huku akiongeza kuwa mashinepewa moja kama hiyo ina uwezo wa kuzalisha urani ya SWU 10 kwa siku.
Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema kiwanda hicho kitaweza kurutubisha urani kwa kiwango cha SWU 190,000 katika kipindi cha miezi 10 ijayo.

SWU ni kifupi cha istilahi ya Separative Work Unit ambayo inahusiana na kiwango cha kasi na uwezo wa kutenganisha urani 235 kutoka urani 237, kiwango ambacho kinaonesha uwezo wa uzalishaji wa mashinepewa (centrifuge) moja.
Iran imechukua hatua hiyo baada ya Marekani kukiuka majukumu yake na kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPO mwezi Mei mwaka huu.