Zarif: Marekani haiwezi kuiweka tena Iran chini ya udhibiti wake
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani hivi sasa inafanya njama kubwa za kuiwekwa Iran chini ya udhibiti wake lakini kamwe haitofanikiwa.
Zarif alisema hayo jana (Jumapili) katika kumbukumbu ya tarehe 19 Agosti iliyosadifiana na siku Marekani ilipofanya mapinduzi ya kijeshi nchini Iran mwaka 1953 na kuipindua serikali ya Dk Mohammad Mosaddiq iliyokuwa imechaguliwa kidemokrasia na wananchi.
Tarehe 19 Agosti 1953, wanajeshi wa utawala wa kifalme wa Shah nchini Iran kwa kushirikiana na Marekani na Uingereza, waliipindua serikali ya Dk Mohammad Mosaddiq na kumrejesha madarakani mfalme Mohammad Reza Pahlavi.
Katika ujumbe wake alioutoa kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema jana kuwa, miaka 65 iliyopita, Marekani iliipindua serikali ya wananchi iliyochaguliwa kidomokrasia nchini Iran na kurejesha utawala wa kidikteta humu nchini na baada ya hapo ikaidhibiti Iran kwa muda wa miaka 25. Hivi sasa pia Marekani imeunda kundi maalumu kwa tamaa ya kufanikisha jambo hilo hilo kupitia mashinikizo, kueneza taarifa za uongo na kudanganya watu, lakini kamwe jambo hilo halitorejea tena nchini Iran.
Wiki iliyopita, Marekani iliunda kundi jingine maalumu la kuendesha kampeni dhidi ya Iran sambamba na mashinikizo ya Washington dhidi ya Tehran.
Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye kabla ya hapo alikuwa Mkuu wa Shirika la Kijasusi la nchi hiyo CIA amesema kuwa, nchi yake infanya juhudi za kuongeza mashinikizo ya pande zote dhidi ya Iran.