Zarif: Hatuna cha kujadili kuhusu makombora ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i4765-zarif_hatuna_cha_kujadili_kuhusu_makombora_ya_iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema katu Jamhuri ya Kiislamu haiwezi kufanya aina yoyote ya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 10, 2016 07:51 UTC
  • Zarif: Hatuna cha kujadili kuhusu makombora ya Iran

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema katu Jamhuri ya Kiislamu haiwezi kufanya aina yoyote ya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora.

Muhammad Javad Zarif, ameyasema hayo katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari na mwenzake Marina Kaljurand wa Estonia mjini Tehran hii leo na kuongeza kuwa, suala la makombora ni suala la ulinzi na usalama wa taifa zima la Iran hivyo Jamhuri ya Kiislamu haiwezi kuzungumza na yeyote yule kuhusu cha kufanya au kutofanya.

Zarif amesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kery, anafahamu fika kuwa Iran ya Kiislamu haiwezi kufanya midahalo na mijadala na mtu au nchi yeyote kuhusu uwezo wake wa makambora.

Kauli ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran inajiri siku chache, baada ya Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kimataifa ambaye pia ni mjumbe mwandamizi katika timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran kusema kuwa hatua ya Iran kuendelea kujiimarisha kiulinzi haikiuki makubaliano ya nyuklia kati ya Tehran na kundi la 5+1.

Kadhalika Mkuu wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran, Ayatullah Sadiq Amoli Larijani siku chache zilizopita alisisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa uwezo wa makombora wa taifa hili. Alisema kuwa, kudhoofisha, kuharibu na kuzitilia alama ya swali juhudi, mafanikio ya kijeshi, kiusalama na kimakombora ya Iran kwa kizingizio cha uhuru wa kutoa maoni ni uhaini na usaliti kwa malengo matukufu ya Jamhuri ya Kiislamu.