Salami: Maadui wa Iran wamedhoofika, Marekani imezidi kutengwa
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesema kuwa, maadui wa Iran wamedhoofika sana na kuongeza kwamba, hivi sasa Marekani imetengwa zaidi kimataifa zaidi ya wakati wowote ule na inahasimiana na nchi kadhaa zikiwemo China, Russia, Canada, Uturuki na Umoja wa Ulaya.
Brigedia Jenerali Hussein Salami ameyasema hayo Alkhamisi katika mji wa Semnan wa mashariki mwa Iran na kuongeza kuwa: "Njama za madola ya kibeberu duniani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu zimegonga mwamba kutokana na mapambano ya taifa la Iran katika kipindi cha miaka 40 iliyopita na kwamba Marekani imetengwa kutokana na mshikamano wa taifa la Iran."
Aidha amesema, chaguo la vita vya kijeshi dhidi ya taifa la Iran haliko kabisa na kuongeza kuwa: "Hakuna nchi iliyo tayari kushirikiana na Washington na hata hiyo Marekani nayo pia haiko katika hali ya kuanzisha vita."
Brigedia Jenerali Salami ameashiria oparesheni ya makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya ngome na kikao cha kundi moja la kigaidi katika eneo lenye mamkalaka ya ndani la Kurdistan nchini Iraq na kusema: "Iwapo adui anakusudia kuichokoza Jamhuri ya Kiislamu, basi Iran itatoa jibu kali."
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa ushindi wa mrengo wa muqawama huko Palestina, Iraq na Syria ni jambo ambalo litapelekea kupatikana mshikamano wa nchi za Kiislamu.
Jumamosi iliyopita Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilijibu hujuma za magaidi wa Kurdistan kwa kuvurumisha makombora saba ya masafa mafupi dhidi ya mkusanyiko wa makamanda wa kigaidi katika eneo la Kurdistan nchini Iraq.