Mapambano dhidi ya ugaidi, Iran haitalegeza kamba
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i48139-mapambano_dhidi_ya_ugaidi_iran_haitalegeza_kamba
Mashambulizi yaliyofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (Sepah) dhidi ya makao ya magaidi huko kaskazini mwa Iraq yameonesha tena kwamba, kinyume na baadhi ya nchi za Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina misimamo ya wazi kuhusu suala la kupambana na ugaidi na kwamba haitalegeza kamba wala kulegalega katika kulinda usalama wa taifa, ardhi yake na vitisho vya kijeshi.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Sep 14, 2018 19:26 UTC
  • Mapambano dhidi ya ugaidi, Iran haitalegeza kamba

Mashambulizi yaliyofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (Sepah) dhidi ya makao ya magaidi huko kaskazini mwa Iraq yameonesha tena kwamba, kinyume na baadhi ya nchi za Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina misimamo ya wazi kuhusu suala la kupambana na ugaidi na kwamba haitalegeza kamba wala kulegalega katika kulinda usalama wa taifa, ardhi yake na vitisho vya kijeshi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi amejibu matamshi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa iliyoeleza wasiwasi wake kuhusu mashambulizi ya Iran dhidi ya magaidi huko kaskazini mwa Iraq kwa kusema kuwa: "Iran ilikuwa tayari imeitahadharisha serikali ya Baghdad na viongozi wa eneo la Kurdistan kuhusu harakati na uharibifu unaofanywa na wanachama wa kundi hilo nchini Iran." 

Bahram Qassemi

Baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kulenga makao na ngome za magaidi huko kaskazini mwa Iraq Jumamosi iliyopita kwa makombora saba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imetoa taarifa ikitaka kuheshimiwa mamlaka ya Iraq na kueleza tena wasiwasi wake kuhusu uwezo wa makombora wa Iran. Msimamo huo wa Ufaransa umeonesha tena jinsi nchi za Magharibi zinavyokabiliana na ugaidi kwa misimamo ya kindumakuwili. Misimamo hii ya kindumakuwili inaonekana wazi zaidi katika mapambano dhidi ya ugaidi nchini Syria. Nchi za Magharibi hususan Marekani, Uingereza na Ufaransa zinapeleka mbele matakwa na malengo yao ya kisiasa kwa kutumia sera za kuugawa ugaidi baina ya ugaidi "mzuri" na ugaidi "mbaya". Kinyume chake, Iran inapinga waziwazi aina zote za ugaidi na kukabiliana nao kwa maneno na kivitendo. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani ugaidi wa aina zote na popote pale unapotokea bila ya kujali mahusiano ya kisiasa na haikubaliani na sera za kindumakuwili katika suala la udharura wa kuheshimiwa mamlaka na ardhi ya nchi nyingine. Ni vyema hapa kueleza kwamba, serikali ya Iran imewatahadharisha mara kadhaa viongozi wa serikali kuu ya Baghdad na wale wa utawala wa Kurdistan kuhusu harakati za makundi ya kigaidi yanayoshambulia ardhi ya Iran kutokea Iraq na kuitaka serikali ya Baghdad ichukue hatua zinazostahili. 

Hata hivyo na licha ya tahadhari hizo, makundi ya kigaidi yaliyoko kaskazini mwa Iraq yalishambulia ardhi ya Iran na kuua raia 11 katika mkoa wa Kurdistan.

Ni wazi kuwa ni haki ya kisheria ya kila nchi kulinda usalama wake wa kitaifa na kujibu harakati kama hizi za kigaidi, na Iran ambayo daima imekuwa mstari wa mbele kukabiliana na ugaidi haiwezi kufumbia jicho au kunyamazia kimya uhalifu kama huu. Kwa msingi huo Jumamosi iliyopita Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) lilivurumisha makombora saba na kulenga makao makuu na mkutano wa viongozi wa kundi moja la kigaidi katika eneo la Kurdistan huko kaskazini mwa Iraq. Mashambulizi hayo yalibeba ujumbe kwamba, Iran haina utani na nchi yoyote katika suala la kupambana na ugaidi na kulinda usalama wake wa kitaifa na itawashambulia magaidi popote pale watakapokuwa. Pili ni kwamba, Iran haihitaji idhini na ruhusa ya nchi yoyote ile kwa ajili ya kulinda ardhi yake na itajibu vitisho vya maadui kwa kutumia nyenzo za kijeshi za uwezo wake wa kiulinzi.

Kuhusu suala hilo, Meja Jenerali Muhammad Ali Ja'fari anasema: "Shambulizi dhidi ya makao ya magaidi huko kaskazini mwa Iraq linabeba ujumbe kwa maadui wote hususan madola makubwa ya kibeberu yanayodhani kwamba, yanaweza kulitia woga na hofu taifa la Iran na kulitwisha matakwa yao machafu."

Meja Jenerali Ja'fari

Meja Jenerali Ja'fari ameongeza kwamba: "Nchi zenye wanajeshi, kambi na zana za kijeshi kandokando ya Iran na katika umbali wa kilomita elfu mbili kutoka ardhi ya Iran zinapaswa kuelewa kwamba, makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) yako makini sana."