Meja Jenerali Jaafari: Wapigania ukombozi duniani wamo katika kuungana dhidi ya Marekani
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) amesema kuwa, watu wanaodhulumiwa pamoja na wapigania ukombozi katika maeneo mbalimbali duniani, hivi sasa wamo katika hali ya kuungana dhidi ya Marekani.
Meja Jenerali Muhammad Ali Jaafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) amesema hayo leo hapa mjini Tehran ambapo amebainisha pia siasa za Marekani na washirika wake ambazo zimepelekea kutokea machafuko, mauaji na uharibifu katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema bayana kwamba, jinai za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za serikali ya Washington na madola yanayounga mkono mfuumo wa kibeberu katu hayatasahauliwa na wananchi wa Palestina, Syria, Iraq na Iran.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) ameongeza kuwa, wananchi wanamapinduzi na wapigania ukombozi wa Yemen kila siku wamekuwa wakishuhudia jinai za Marekani na washirika wake zikiwemo za kumwagwa damu ya wanaume, wanawake na watoto madhulumu na wasio na hatia wa nchi hiyo.
Meja Jenerali Muhammad Ali Jaafari amesisitiza kuwa, moja ya mambo muhimu ya utamaduni wa kila Muirani ni nguvu, uwezo sambamba na kuchukia dhulma.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) ameongeza kuwa, madhali dhulma ya mfumo wa kimabavu ukiongozwa na mfumo wa ubeberu wa Marekani uungalipo, basi siasa za Iran mkabala na madola hayo hazitabadilika.