Brigedia Jenerali Salami: Marekani haina uwezo wa kupambana kijeshi na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49713-brigedia_jenerali_salami_marekani_haina_uwezo_wa_kupambana_kijeshi_na_iran
Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kwamba, matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani, Donald Trump, yanaonyesha kukata tamaa na woga wa hali ya juu ilionao nchi hiyo katika kukabiliana kijeshi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Nov 23, 2018 23:16 UTC
  • Brigedia Jenerali Salami: Marekani haina uwezo wa kupambana kijeshi na Iran

Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kwamba, matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani, Donald Trump, yanaonyesha kukata tamaa na woga wa hali ya juu ilionao nchi hiyo katika kukabiliana kijeshi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Brigedia Jenerali Hossein Salami aliyasema hayo jana (Ijumaa) katika kongamano la mkoa wa Gilan, kaskazini mwa Iran na kuongeza kwamba mataifa ya Kiislamu yamepata ilham ya kujifunza kutoka katika sifa ya kujitolea ya wananchi wa Iran, kusimama kwao kidete na muqawama wao ambao matokeo yake yatakuwa ni kuifanya Marekani na waitifaki wake kuondoka kwa udhalili katika ardhi za Waislamu. Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amefafanua kwamba uhuru na kujitawala mataifa yanayodhulumiwa na kufikia kujiainishia  yenyewe mustakbali na uhuru wao, ni mambo ambayo yametokana na kupanuka fikra ya kujitolea ya wananchi wa Iran.

Brigedia Jenerali Hossein Salami, Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la SEPAH (IRGC) 

Aidha amesisitiza kwamba ni jambo lisilowezekana kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani na vibaraka wake kama vile utawala haramu wa Kizayuni. Ameashiria kuwa, kushindwa utawala wa Saudi Arabia huko nchini Yemen na pia matamshi hayo hayo ya kila siku ya utawala khabithi wa Israel kuhusiana na makombora ya Harakati ya Kiislamu ya HAMAS pamoja na kushindwa Marekani katika medani ya vita, yote hayo ni katika ahadi zinazothibiti za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Aidha ameelezea umuhimu wa kupanuliwa utamaduni wa kujitolea kwa mataifa yote ya Kiislamu, kuanzia Palestina, Lebanon, Iraq, Syria na Yemen na kusisitiza kwamba, kipindi cha kupora utajiri wa mataifa ya Kiislamu na kutwaa raslimali zao kunakofanywa na Marekani kinakaribia kufika mwisho kutokana na baraka za kujitolea kimapambano za wananchi wa Iran. Jumanne iliyopita rais wa Marekani aliituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba eti inachafua usalama wa eneo la Mashariki ya Kati sambamba na kuwavunjia heshima wananchi wa Iran.