Uwezo wa Jeshi la Majini la Iran kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu
Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran jana alikutana na makamanda na wakuu wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kumepatikana mafanikio makubwa katika Jeshi la Iran hasa jeshi la majini tokea mwanzo wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi sasa.
Katika mkutano huo ambao ulifanyika kwa munasaba wa Siku ya Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Kiongozi Muadhamu aliashiria jinsi kambi kubwa ya maadui na washindani ilivyojipanga kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba: Kuwepo kwa hali hii halisi sambamba na udharura wa kufidia hali ya kubaki nyuma kimaendeleo, vinadhihirisha ulazima uliopo wa kuchapa kazi kwa kiwango cha juu zaidi ya kawaida katika sekta zote za Jamhuri ya Kiislamu ikiwemo ya Jeshi la Majini."
Aidha aliendelea kusema: "Ongezeni kiwango cha uwezo wenu na utayari wenu kadiri mnavyoweza ili maadui wa Iran wasiwe na uthubutu hata wa kutoa vitisho dhidi ya taifa adhimu la Iran."
Katika zama za Kujihami Kutakatifu kuanzia mwaka 1980 hadi 1988, Jeshi la Majini la Iran liliweza kuleta fahari kubwa ambayo imedumu katika kumbukumbu. Leo pia Jeshi la Majini la Iran, kwa kutegemea imani, na nguvu kazi ya vijana wenye ubunifu na kwa kutumia uzoefu wenye thamani wa zama za kujihami kutakatifu, limeweza kuwa na nafasi muhimu sana katika kulinda mipaka ya majini na pia kulinda doria na kudumisha usalama katika maji ya kimataifa. Jeshi hilo limeeneza pia satwa yake katika eneo muhimu la Pwani ya Makran, Bahari ya Oman na maeneo ya mbali zaidi ya maji ya kimataifa.
Jeshi la Mjini la Iran limetekeleza kazi muhimu baharini na limeweza kutuma manowari zake kulinda doria na kudumisha usalama katika maji huru katika Bahari ya Hindi, Lango Bahari la Babul Mandab, Mfereji wa Suez na Bahari ya Mediterranea.
Azma ya Jeshi la Majini la Iran iko katika kuendeleza ustawi katika nyuga za ulinzi na kuonyesha uwezo wake wa kumzuia adui. Kama ambavyo Kiongozi Muadhamu alivyosema: "Kizazi cha sasa cha jeshi la wanamaji kina imani ya dhati kwa ubunifu na vipawa kilivyonavyo; na kujumuishwa manowari angamizi ya Sahand na nyambizi za Fateh na Ghadir kwenye vyombo vya jeshi la wanamaji kunatoa bishara ya uwezekano wa kupatikana maendeleo zaidi kadiri siku zinavyosonga mbele. Hakuna sahaka kamba, kuwa tayari zaidi vikosi vya ulinzi vya Iran kutalipa kinga taifa ya kutoweza kushambuliwa na kuwatia hofu maadui na hilo ni jambo la dharura katika kulinda usalama mkabala wa vitisho."
Kituo cha Utafiti wa Kistratijia cha Tabyin, katika makala iliyochambua uwezo wa majaeshi ya majini katika kuzuia maadui, limeashiria nukta hii kuwa: "Moja ya nukta za kimsingi katika kuibua uwezo wa kuzuia adui baharini ni kumiliki teknolojia ambayo inatumika katika uundaji zana za kivita zinazotumika baharini. Hizi ni teknolojia kama vile mfumo wa ubaharia wa kielektroniki, kuunda manowari na nyambizi zinazoweza kubakia muda mrefu baharini, kuimarisha uwezo wa vita vya kielktorniki baharini na pia kuwa na makombora yanayoweza kuongozwa ili kulenga shabaha kwa ustadi."
Uzoefu wa takribaini karne moja unaonyesha kuwa, usalama wa eneo hasa katika Ghuba ya Uajemi unapapswa kuwa mikononi mwa nchi za eneo. Hii ni kwa sababu uingiliaji na uwepo wa majeshi ajinabi katika eneo ni chanzo cha ukosefu wa amani na migogoro. Uingiliaji wa madola ya ajinabi unatokana na umuhimu wa kistratijia wa eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati. Aidha madola hayo yanalenga kuzifanya nchi za eneo hili ziwe tegemezi kiusalama na kwa njia hiyo zinunue silaha zenye kugharimu mabilioni ya dola ili kulinda usalama wao.
Kwa msingi huo jeshi la majini lina nafasi muhimu na ya kistratijia katika kulinda usalama. Kama alivyosema Amiri Jeshi Mkuu: "Jamhuri ya Kiislamu haikusudii kuanzisha vita dhidi ya mtu yeyote lakini inapaswa kuongeza na kuimarisha uwezo wake ili si tu adui awe na woga na hofu ya kuishambulia Iran, lakini kwa baraka za mshikamano, nguvu na uwepo athirifu wa vikosi vya ulinzi katika medani, wingu la vitisho pia liwe mbali na anga ya taifa la Iran."